tuwasiliane

Monday, April 23, 2012

23 APR. Mbunge atishwa kwa kutumia SAINI yake


Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola, alipigiwa simu juzi saa saba za usiku na kiongozi mmoja wa juu wa CCM akimtaka ajiandae kwa mapambano kwa kile kilichoelezwa kuwa amekisaliti chama.

Akithibitisha tukio hilo, Lugola alisema kuwa kiongozi huyo mzito (jina tunalo) ambaye ni bingwa wa kufoka na kutukana vyombo vya habari vinavyomkosoa, alimwita mbunge huyo mnafiki, mzandiki na kwamba kwa hatua yake ya kusaini hoja ya kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu atambue kuwa ametangaza vita.

“Ni kweli nilipigiwa simu na..(anamtaja) na kuanza kunifokea na kunitukana. Nilishindwa kuamini kama kiongozi mzito kama yeye anaweza kuniambia maneno hayo. Nami nilimwambia kwa kuwa sina kosa na nimetumia haki yangu, afanye lolote analoweza.”

Mbunge huyo alisema pamoja na kuambiwa kuwa leo kigogo huyo wa CCM atafika Dodoma kumshughulikia na wale wote tuliotia saini, haogopi lolote na yuko tayari kukabiliana na magumu kwa ajili ya maslahi ya Watanzania.

“Hata wakiniua, sitaogopa naamini katika ukweli na ni kilio cha wengi. Lakini wengi wananiunga mkono, na wamenipigia simu na wanakubali kuwa wako nyuma yangu.

Alisema maisha ya Watanzania ni mabaya, shuleni hakuna walimu wala madawati, hospitali ziko taabani kwa kukosa dawa huku madaktari wakililia maslahi, na kila wakati serikali imekuwa ikidai haina fedha kumbe, zipo na zinaliwa na wajanja.

“Hakuna cha kunitisha katika hali kama hii. Wanaonitisha ndiyo wasioitakia mema CCM na Watanzania na hao lazima tuwashughulikie mchana kweupe. Na katika hili, lazima wote bila kujali wao ni nani lazima wajiuzulu bila kusubiri eti wajipime na kutafakari,” alisema Lugola.

SOURCE. DARHOTWIRE

No comments:

Post a Comment