tuwasiliane

Friday, April 20, 2012

20 APR. WABUNGE KUMPIGIA KURA YA KUTOKUWA NA IMANI NA WAZIRI MKUU


WABUNGE wameendelea kuwasulubu mawaziri wakiwatuhumu baadhi yao kuhusika na ubadhirifu wa fedha za Serikali huku Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe akisema ana ushahidi unaoonesha kuwa wengi wa viongozi hao wa wizara ‘wanaitafuna’ nchi.

Tuhuma hizo, zilisababisha Mnadhimu Mkuu wa Shughuli za Serikali Bungeni, William Lukuvi kusimama na kutaka ushahidi huo na orodha ya majina ya mawaziri husika viwasilishwe kwa Spika.

Mbunge huyo alitoa hoja hiyo jana wakati wa mjadala juu ya ripoti tatu za Kamati za Bunge za Mashirika ya Umma (POAC), Serikali za Mitaa (LAAC) na Hesabu za Serikali Kuu (PAC).

Aidha wabunge wametaka waongezewe siku mbili bila posho wajadili kwa undani taarifa hizo.

Filikunjombe alisema hayo baada ya kuomba Mwongozo wa Naibu Spika, Job Ndugai, juu ya mchango wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami aliyefafanua juu ya sakata la Shirika la ViwangoTanzania (TBS) kwa kusisitiza kuwa Wizara yake haimkingii kifua Mkurugenzi, Charles Ekelege, kama wanavyosema wabunge.

“Waziri anapolidanganya Bunge, achukuliwe hatua gani? Waziri Chami anasema alitekeleza maelekezo yote ya PAC, kwamba uchunguzi unapofanyika Mkurugenzi wa TBS akae pembeni. Uchunguzi umefanyika Mkurugenzi akiwa kazini…tuna ushahidi wa kutosha, kwamba wanaoongoza ‘kutafuna’ nchi hii ni mawaziri wenyewe na nitataja mmoja mmoja kwa majina na ushahidi tunao,” alisema Filikunjombe.

Waziri Lukuvi alisimama na kusema: “Ningeelewa kama angejenga hoja kuona kama Waziri Chami alidanganya…kuhitimisha kwamba mawaziri wote ni wezi, athibitishe. Naomba akukabidhi (Naibu Spika) wizi uliofanywa wa kila waziri aliye katika Bunge.” Hata hivyo, Filikunjombe alisimama tena na kusema ni mawaziri wengi na akasisitiza kutoa ushahidi. Dk. Chami katika kuchangia mjadala, alisema ikibainika kuwapo mtu, ndugu au rafiki mwenye kampuni hewa au maslahi binafsi katika ukaguzi wa magari nje ya nchi, ataweka uwaziri wake rehani kwa kujiuzulu.

“Haina maana, nitaamua kumfukuza kazi mteule wa Rais bila kufuata utaratibu? Nimekosea wapi? Kwamba mimi namlinda Mkurugenzi?” Alihoji na kusisitiza kwamba hakuna mtu atakayelindwa au kukingiwa kifua asichunguzwe.

Mbunge wa Singida Magharibi, Tundu Lissu (Chadema), aliwataka wabunge kuanzisha mjadala wa kutokuwa na imani na Serikali. Alisema kila mwaka taarifa ya CAG imekuwa ikionesha wizi mkubwa uliofanyika, lakini hakuna waziri anayewajibika kwa wizi unaofanyika katika wizara.

“Hatujawahi kuona mtendaji akichukuliwa hatua. Hatujaona Waziri akiwajibika kwa sababu ya wizi katika wizara yake au sababu ya kuhusishwa na uvundo wa wizi wa fedha za umma,” alisema Lisu na kuongeza kuwa wapo wanaotaka ubunge ili wawe mawaziri kwa lengo la kupora.

Hata hivyo, Lisu alisema hoja yake ya kutaka mjadala wa kutokuwa na imani ya Serikali na Waziri Mkuu, si kwamba ana hila na Mizengo Pinda, isipokuwa ni kwa sababu ya mfumo wa utawala uliopo.

“Tuna uwezo kusema Waziri Mkuu wajibika kwa madudu ya Serikali yako,” alisisitiza. Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed aliwataka wabunge watumie mamlaka waliyopewa na Katiba, kuhakikisha wanawajibisha wasiotaka kuwajibika. Alisema Katiba inawapa mamlaka ya kutumia asilimia 30 kuishauri Serikali na iliyobaki ni kuidhibiti.

“Asilimia 70 tumeshafanya muda mrefu, sasa tutumie kudhibiti madhambi yasiyopatiwa ufumbuzi,” alisema.

Akizungumzia taarifa ya CAG iliyoonesha kuwapo mishahara hewa iliyolipwa katika baadhi ya vyuo vikuu, Mbunge wa Viti Maalumu, Christowaja Mtinda (Chadema) aliitaka Serikali itoe maelezo ni nani anapokea fedha hizo.

Mtinda ambaye alipinga makatibu wakuu kupewa nyumba Dodoma na kuzitumia kipindi cha mikutano ya Bunge pekee, alisema katika kupitia taarifa za mwaka za Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) alikuta jina lake kwenye orodha ya watumishi wa chuo hicho, licha ya kwamba hajawahi kufanya kazi katika taasisi hiyo.

Mbunge wa Viti Maalumu, Aina Mohamed Mwidau (CUF), aliendelea kuhoji mkataba wa ukodishaji ndege kwa kuhoji Menejimenti ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) iliyokuwapo ilipata wapi kiburi cha kuchukua uamuzi huo wakati timu ya wataalamu ilisema si busara kufanya hivyo.

Mbunge wa Lulindi, Jerome Bwanausi (CCM) alitaka halmashauri zinazotuhumiwa na ubadhirifu wa fedha za umma, wakurugenzi na watendaji wasimamishwe mara moja.

Hata hivyo, Mbunge wa Shinyanga Mjini, Steven Masele (CCM) licha ya kueleza kusikitishwa na ripoti za CAG kutofanyiwa kazi, alisema wapo mawaziri na wakurugenzi wanaofanya kazi nzuri isipokuwa wanaangushwa na Wizara ya Fedha kwa kuwapa fedha kidogo tofauti na bajeti.

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri, akichangia mjadala alitangaza ‘vita’ kwenye halmashauri na kusema itakapoanza, Serikali haitataka suluhu.

“Tuachieni, msitushike mkono. Tutaandaa vita katika jambo hili ili kutatua tatizo la msingi,” alisema na kusisitiza kwamba wataingia pia kwenye halmashauri zenye hati safi kuangalia thamani ya fedha na kwamba kwa wenye hati chafu, Katibu Mkuu ameshaagizwa wakurugenzi watendaji wawajibishwe.

Naibu Waziri wa Fedha, Pereira Ame Silima akichangia mjadala, alisema imeundwa timu kwenda halmashauri zote kufuatilia mishahara hewa. Alikiri kuwepo tatizo hilo na watendaji wanaojihusisha huku akisema baada ya taarifa, hatua zitachukuliwa kwa wahusika.
WAKATI HUOHUO MH ZITTO KABWE ALISEMA JANA KUWA KUANZIA LEO ATAKUSANYA SAIN ZA WABUNGE 70 TU ILI KUWEZA KUPIGA KURA YA KUTOKUWA NA IMANI NA WAZIRI MKUU. ILI KUEPUSHA HILO ZITO AMETOA WITO KWA WABUNGE AMBAO WAMEHISIKA NA SAKATA LA UFISADI

No comments:

Post a Comment