tuwasiliane

Wednesday, April 18, 2012

18 APR. YANGA YAUTEMA UBINGWA


Simba imendelea kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania baada ya kuichapa JKT Ruvu kwa mabao 3-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.
Kwa matokeo hayo, Simba imejiweka katika nafasi nzuri ya kunyakua ubingwa huo baada ya kujikita zaidi kileleni mwa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 56 ikiwazidi, pointi 13 mabingwa watetezi, Yanga.
Simba ilianza kwa kasi mchezo na kufanikiwa kupata bao la kwanza katika dakika ya kwanza ya mchezo lililofungwa na Uhuru Selemani kwa kichwa baada ya kuunganisha kona iliyopigwa na Emnuel Okwi.
Simba walizidi kulisakama lango la JKT Ruvu ambapo katika dakika ya saba, Amir Maftah alitoa pasi ambayo Seleman alichelewa kuunganisha na kutoka nje.
Simba waliendelea kulisakama lango la JKT ambapo katika dakika ya 17, Haruna Moshi ‘Boban’ aliipatia timu yake bao la pili baada ya uzembe uliofanywa na Emanuel Pius wa JKT na kupachika wavuni mpira.
Wekundu hao wa Msimbazi, walifanya mashambulizi tena katika dakika ya 26 ambapo Seleman alikosa bao baada ya kupaisha juu mpira aliopasiwa na Maftah huku Gervas Kago naye akikosa akikosa bao baada ya kushindwa kumalizia pasi ya Seleman katika dakika ya 39.
JKT walicharuka na kuliandama lango la Simba ambapo katika dakika ya 42, Hussein Bunu alikosa bao baada ya kushindwa kumalizia pasi ya Pius.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikijaribu kusaka bao, lakini katika dakika ya 64, Mwinyi Kazimoto aliipatia Simba bao la tatu baada ya kuachia shuti kali lililomshinda kipa wa JKT, Aman Simba.
JKT walifanya mabadiliko katika dakika ya 71 kwa kutoka Mohamed Banka na nafasi yake kuchukuliwa na George Mketo.
Kwa upande wa Simba alitoka Juma Nyoso na kuingia Obadia Mungusa, huku Kago akitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Edward Christopher.

Kwa upande mwingine mambo yamezidi kuwa mabaya kwa klabu ya Yanga baada ya kupokea kipigo kingine kutoka kwa Kagera Sugar leo hii katika uwanja wa Kaitaba.

Goli la Kagera lilifungwa na Shija Mkina katika kipindi cha kwanza cha mchezo., na mpaka filimbi ya mwisho inalia Kagera 1-0 Yanga.

No comments:

Post a Comment