Wednesday, April 18, 2012
18 APR. SIMBA,YANGA VITANI LEO
BAADA ya kuduwazwa na kipigo cha mabao 3-2 toka Toto Africans wiki iliyopita, mabingwa Yanga wanashuka dimbani leo kusaka tiba ya kuwarejesha kwenye mstari wa mbio za ubingwa Ligi Kuu Bara pale watakaposugua nyasi za Uwanja wa Kaitaba, Bukoba dhidi ya wenyeji Kagera Sugar walioapa kuhakikisha mabingwa hao wanaondoka Kanda ya Ziwa bila pointi.
Mbali na jaribio hilo la Yanga ambayo itamkosa beki wake Chacha Marwa aliyefiwa na mtoto wake leo, jijini Dar es Salaam vinara, Simba watakuwa na kibarua cha kujiimarisha kileleni watakapowavaa JKT kwenye Uwanja wa Taifa.
Yanga inayoonekana kupotea kwenye safari ya ubingwa, italazimika kushinda ili angalau kurejesha matumaini, lakini pia ikiomba Simba na Azam zinazofukuzaka katika nafasi ya kwanza na pili zifanye vibaya kwenye mechi zilizosalia.
Kama itashinda mechi zake zote zilizobaki basi itafikisha pointi 55, ambazo Simba wenye pointi 53 wanahitaji ushindi kwenye mchezo mmoja tu kuzivuka, huku Azam yenye pointi 50, ikihitaji ushindi wa michezo miwili tu kuzipiku.
Lakini endapo watashinda rufaa yao dhidi ya Coastal Union na kurudishiwa pointi, watafikisha 58 ambazo hata hivyo italazimika kusubiri kudra za mwenyezi Mungu, kwani Simba ikishinda mechi zake mbili na Azam tatu zijazo zinavuka pointi hizo.
Wafuatiliaji wa Ligi Kuu wanatabiri kwamba mechi zote mbili zitakuwa na mvuto wa aina yake hasa ukizingatia historia nzuri ya kuharibu mipango ya vigogo hivyo vya soka la Tanzania ilizonazo timu za Kagera na JKT.
Katika michezo ya duru la kwanza, Simba iliishinda JKT mabao 2-0, huku Yanga ikiichapa Kagera bao 1-0. Hiyo ina maana kwamba mechi hizo za marudiano kwa vigogo hao zitakuwa na upinzani mkubwa.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Fredy Minziro amesema atafanya mabadiliko kwenye kikosi chake cha kwanza ili kiweze kuendana na hali halisi ya ushindani kuelekea mwishoni mwa msimu.
Kwa upande wake, Kocha wa Simba, Milovan Circovic amesema dhamira yake ni ushindi na kikosi chake hakitakuwa na mzaha kwenye mechi hiyo zaidi ya kuondokana pointi zote tatu.
Kocha wa JKT Ruvu Charles Kilinda alisema: "Simba ni nzuri, lakini kamwe hatuwezi kuwa daraja kwao, lengo letu ni kulipa kiasi na uwezo huo tunao."
Burudani ya ligi hiyo pia itakuwa Kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza ambako wenyeji Toto Africans wataonyeshana wataonyesha kazi na African Lyon, wakati maafande wa Ruvu Shooting watakuwa kwenye Uwanja wa Mabatini kupepetana na Moro United.
Mechi nyingine itakuwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma kati ya wachovu Polisi Dodoma wanaokamata mkia kwenye msimamo wa ligi watakapoumana na Coastal Union ya Tanga.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment