Friday, April 13, 2012
13 APR.Azam FC yatua Dodoma, Under 20 washinda Zanzibar
Kikosi cha Azam FC kimetua mkoani Dodoma kwa ajili kucheza mchezo mmoja dhidi ya Polisi Dodoma utakaochezwa siku ya Jumamosi kwenye uwanja wa Jamhuri.
Azam FC iliondoka DSM na wachezaji wote 24 isipokuwa Aishi Salum aliyekwenda kujiunga na kikosi cha timu ya taifa, kesho Azam FC itafanya mazoezi katika uwanja wa Jamhuri.
Akizungumza na tovuti ya www.azamfc.co.tz Mapema kabla ya kuondoka kocha wa Azam Stewart Hall amesema timu inaenda Dodoma mapema ili kupata muda wa kufanya mazoezi katika uwanja huo unaotofautiana na uwanja wanaotumia wa Azam Chamazi.
Stewart alisema wanaenda Dodoma wakiwa wamejiandaa vya kutosha kuweza kupata pointi tatu muhimu zitakazowaweka vizuri katika harakati za kusaka nafasi mbili za juu.
“Safari yetu tunaomba iwe yenye heri, tunatarajia kupata pointi tatu kwa kuwa tupo vizuri na wachezaji wote wamejiandaa na wana ari ya kimchezo japo tutakuwa ugenini”
Alisema wameamua kuondoka na wachezaji wote kwakuwa kikosi cha timu ya vijana Academy kipo visiwani Zanzibar, hivyo wachezaji watakaobaki hawatakuwa wanafanya mazoezi, wanaondoka wakafanye mazoezi na wenzao.
Akielezea hali ya wachezaji wenye majeruhi Abdi Kassim ‘Babi’ na Joseph Owino, kocha alisema nao watakuwa katika msafara huo kwa kuwa wanafanya mazoezi ya taratibu.
Wakati huo huo, Azam Academy jana iliwasili salama visiwani Zanzibar kwenye kambi ya siku nne, na leo wamecheza mchezo wake wa kwanza na Kilimani City inayoshiriki ligi daraja la pili na kuifunga 2-1 kwenye uwanja wa Ngome. Magoli ya vijana yakifungwa na Mudhhatir Yahya na Joseph Kimwaga.
Kesho Kikosi cha Vivek Nagul kitakwaana na kikosi cha Zanzibar Under 17
Kikosi kilichopo Dodoma ni, Mwadini Ally, Agrey Moris, Erasto Nyoni, Said Morad, Wazir Salum, Haji Nuhu, Abdulhalim Humud, Abdi Kassim, Jabir Aziz, Salum Aboubakar na Michael Bolou Kipre.
Wengine ni Herman Tchetche Kipre, John Bocco, Gaudence Mwaikimba, Himid Mao, Ibrahim Shikanda, Luckson Kakolaki, Abdulghan Gulam, Ibrahim Mwaipopo, Khamis Mcha, Mrisho Ngassa na Zahor Pazi. Joseph Owino na Juckson Wandwi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment