Tuesday, April 10, 2012
10 APR. Kilichomuua Kanumba ni Brain Concussion!
Siku chache baada msiba wa staa wa filamu Steven Kanumba, kulistua Taifa, taarifa za kitabibu zinaweka wazi kuwa kilichomuua msanii huyo ni mtikisiko wa ubongo linalojulikana kitalaamu kama Brain Concussion.
Taarifa zilizopatikana baada ya jopo la madaktari bingwa watano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu huyo, zimeeleza kuwa tatizo hilo linaweza kumfanya mtu apoteze maisha mara moja.
Mmoja wa madaktari hao alisema waligundua tatizo hilo baada ya kumfanyia uchunguzi huo kwa zaidi ya saa mbili.
“Tulianza kuufanyia uchunguzi mwili wa marehemu kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 6:45 mchana na tukagundua kuwa marehemu alifariki kutokana na mtikisiko wa ubongo kwa kitaalamu, Brain Concussion,” alisema daktari huyo. Alisema Kanumba alipata mtikisiko wa ubongo ambao husababisha kufeli kwa mfumo wa upumuaji (cardio-respiratory failure) “Kilichomuua hasa ni mtikisiko wa ubongo, ambao endapo unatokea katika sehemu ya nyuma ya ubongo (cerebrum), huua kwa haraka” alisema daktari huyo na kuongeza kuwa mtikisiko wa ubongo wa nyuma, husababisha matatizo ya mfumo wa upumuaji na hilo limeonekana katika mwili wake.
“Baada ya ubongo wake kutikiswa kwa nguvu, mfumo wa upumuaji ulifeli na ndiyo maana tumekuta kucha za Kanumba zikiwa na rangi ya bluu, huku mapafu yake yakiwa yamevilia damu na kubadilika kuwa kama maini.
Hizo ndizo dalili za kufeli kwa mfumo wa upumuaji.”
“Mtu aliyepata mtikisiko wa ubongo huweza kutokwa na mapovu mdomoni na hukoroma kabla ya kukata roho na ndivyo ilivyokuwa kwa Kanumba kabla hajafariki.”
Daktari mwingine aliyeshiriki katika uchunguzi huo alisema ubongo wa mwigizaji huyo ulikuwa umevimba na kushuka karibu na uti wa mgongo na hivyo kuathiri mfumo wa upumuaji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment