MWANAFUNZI wa darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Mtendeni Dar es Salaam, Maggid Said (7), amekufa baada ya kuchomoka kwenye basi kupitia dirishani likiwa kwenye mwendo na kuanguka barabarani na kupasuka kichwa.
Maggid alidondoka kutoka ndani ya basi hilo na kufikia kwenye lami alipokuwa anacheza na wenzake ndani ya basi hilo ambalo ni daladala linalotumika kusafirisha wanafunzi.
Kutokana na ajali hiyo, Polisi imepiga marufuku mabasi yote ya shule kubeba wanafunzi bila msimamizi wa wanafunzi na yeyote atakayebainika kwenda kinyume na amri hiyo, atachukuliwa hatua za kisheria.
Kwa mujibu wa Polisi basi hilo lililokuwa na wanafunzi wa shule za Mtendeni na Olympio ni daladala linalofanya safari kati ya Temeke na Kariakoo na halikuwa na msimamizi wa wanafunzi hao. Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (SUMATRA) imelaani daladala kubeba wanafunzi kuwa ni kinyume na utaratibu wa Mamlaka hiyo na kuahidi kulichukulia hatua basi hilo na mmiliki wake.
Akizungumza jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, alisema ajali ya Maggid aliyezikwa jana Mbagala, ilitokea juzi saa sita mchana katikati ya Jiji kwenye makutano ya barabara za Indira Gandhi na Uhuru.
Alisema wanafunzi hao wakiwa kwenye basi hilo Toyota Costa namba T 522 AGS, Maggid na wenzake waliokaa kwenye kiti cha nyuma, walikuwa wanacheza huku madirisha yakiwa wazi ndipo Maggid alipochomoka na kuanguka barabarani.
“Alifikia kichwa na kujeruhiwa kichwani na kukimbizwa hospitalini, lakini alifariki dunia Muhimbili,” alisema Shilogile na kukanusha taarifa zilizosambaa kuwa mtoto huyo alianguka barabarani kupitia tobo kwenye sakafu ya daladala hilo.
Alisema si kweli kuwa gari hilo lilitoboka, kwani lilikaguliwa na askari na kubainika kuwa Maggid alikutwa na mauti baada ya kuchomoka dirishani upande wa kulia na mashuhuda wa tukio hilo walimkimbiza hospitalini.
Alisema kitendo cha daladala kubeba wanafunzi si tatizo, ila tatizo ni kukosekana msimamizi ndani ya basi, hali ambayo si salama kwa wanafunzi hao.
“Na ndiyo maana tunasisitiza kuanzia sasa basi la shule lisilo na msimamizi likamatwe.”
Shilogile alisema dereva wa daladala hilo alitoroka baada ya ajali, lakini alisahau leseni yake ya udereva na kumtaja kuwa ni mkazi wa Temeke, aitwaye William Komba na kondakta wake, Mohammed Kahubo anashikiliwa na Polisi.
Sumatra waja juu Ofisa Mfawidhi Kanda ya Mashariki wa Sumatra, Conrad Shio, alisema siku zote Mamlaka hiyo imekuwa ikipigia kelele mabasi ya shule kutambuliwa kwa alama kama mabasi mengine na kuwa na msimamizi maalumu wa wanafunzi.
“Kazi ya msimamizi huyu pamoja na kusimamia usalama wa wanafunzi ndani ya basi pia atasimamia hata wanapofika vituoni na kuvuka barabara salama na kuhakikisha wanafika majumbani mwao salama pia,” alisema.
Aidha alisema Mamlaka hiyo iliagiza pamoja na mabasi hayo ya shule kutambuliwa kwa rangi, lakini pia madirisha lazima yapitishwe nondo katikati, jambo ambalo kwa daladala si rahisi kufanyika.
“Kuhusu tukio hili, leo (jana) asubuhi nimeongea na Ofisa Polisi wa Kanda (ZPO), tumemwambia wakimaliza shughuli zao za kipolisi kuhusu tukio hili, Sumatra nasi tutachukua hatua zetu dhidi ya daladala hilo,” alisema.
Familia yaomboleza Mjomba wa Maggid, Salim Said, alisema basi lililokuwa limebeba wanafunzi hao lilikodiwa na si la shule. Akizungumza kwa uchungu wakati akiandaa mwili wa Maggid kwenye mochari ya Muhimbili alisema si kweli kwamba gari hilo lilikuwa na tundu ila mtoto huyo alichomokea dirishani upande wa dereva.
Alisema Maggid alikuwa akiishi na mama yake mzazi, Mbagala, na wazazi wa wanafunzi wa shule hizo ndio waliokodi gari hilo kwa ajili ya kuwapeleka na kuwarudisha nyumbani. Kwa mujibu wa Said, baada ya kupokea taarifa za kifo cha Maggid juzi saa 8:45 mchana, aliomba namba ya simu ya dereva wa gari hilo, akapewa na alipompigia aliambiwa mtoto huyo kachomokea dirishani na kukimbizwa hospitalini.
Hata hivyo, alisema alifika Muhimbili na alipouliza Mapokezi alithibitishiwa kuwa mtoto huyo alifika akiwa ameshakata roho. Juzi kupitia kipindi cha Jahazi, kituo cha redio cha Clouds FM, kilitangaza tukio hilo, huku kikisema alidondoka kwa kupitia tundu kubwa lililojitokeza katika sakafu ya basi hilo.
SOURCE HABARI LEO
No comments:
Post a Comment