tuwasiliane

Sunday, March 25, 2012

25 MARCHI. SIMBA KAZI NI KAZI TU LEO


WAWAKILISHI wa Tanzania k w e n y e michuano ya kimataifa, Simba leo watakuwa na kazi ngumu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam watakapocheza na timu ya ES Setif kutoka Algeria kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

Simba ilifanikiwa kuingia kwenye hatua hiyo, baada ya kuiondosha Kiyovu ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-2.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Kigali, timu hizo zilitoka sare ya kufunga bao 1-1, kabla ya Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye mchezo wa marudiano.

Mchezo wa leo ni mgumu kwa timu zote, kwani timu yoyote itakayoibuka na ushindi itajiweka kwenye mazingira mazuri zaidi katika mechi ya marudiano wiki mbili zijazo.

Simba wanatakiwa kuibuka na ushindi wa mabao mengi kwenye mchezo wa leo, ili kujiweka kwenye mazingira mazuri zaidi katika mchezo wa marudiano.

Kwani Simba ina faida moja ya kucheza kwenye uwanja wa nyumbani mbele ya mashabiki wake, na hivyo iwapo wataibuka na ushindi mzuri, watakuwa na kazi rahisi kwenye mchezo huo wa marudiano.

Tayari kocha wa SE Setif, Alain Geiger amesema kwamba anatarajia mchezo wa leo utakuwa mgumu kutokana na rekodi nzuri ya Simba kwenye mechi za kimataifa.

Geiger, ambaye ni beki wa zamani wa timu ya taifa ya Uswisi, amesema historia ya Simba ya kuivua ubingwa wa Afrika Zamalek mwaka 2003 jijini Cairo, Misri, ndiyo inayowatisha zaidi.

Kwa upande wa Simba, nahodha wa timu hiyo Juma Kaseja akiizungumzia mechi hiyo alisema
anatarajia watawapa raha Watanzania kwani ndio wanachokitaka kutoka kwa wawakilishi wao hao.

Alisema, Simba pekee ndio imebaki kwenye michuano ya kimataifa kwa upande wa klabu hivyo wana kila sababu ya kupigana kufa kupona kuhakikisha wanawafurahisha Watanzania.

“Hakuna lisilowezekana kama ushirikiano ukiwa nje na ndani ya uwanja, tunaomba sana ushirikiano wa mashabiki maana hamasa yao itasaidia tuwamalize mapema wapinzani wetu,” alisema.

Baada ya mechi hiyo Simba itakuwa ugenini Aprili 6 katika mechi ya marudiano na endapo itafanikiwa kusonga mbele, itacheza mechi ya kwanza nyumbani Aprili 29 na mshindi kati ya El Ahly Shandy ya Sudan na Ferroviario de Maputo ya Msumbiji na mechi ya marudiano itachezwa kati ya Mei 11, 12 na 13.

No comments:

Post a Comment