
MABINGWA watetezi, Yanga leo watarudi kwenye nafasi yao ya pili kama watafanikiwa kuichapa Villa Squad katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara utakaofanyika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Yanga ina pointi 40 baada ya kucheza michezo 19, ikiwa nyuma ya Azam kwa pointi moja na nne kwa vinara wa ligi Simba wenye pomti 44, ambapo Azam watashuka dimbani kesho kuikabili Ruvu JKT huku Simba ikicheza na Mtibwa Sugar.
Pamoja na Yanga kuwapoteza nyota wake kadhaa, katikati ya wiki hii ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya African Lyon na kurudisha matumaini yao kwamba wanaweza kutetea taji lao.
Mabingwa hao watetezi wataingia uwanjani wakiwa na tumaini la kuendeleza kasi ya ushindi dhidi ya vibonde wa ligi Villa Squad yenye pointi 16 ambayo inaonekana kama imekubali kushuka daraja msimu huu.
Kocha wa Villa, Habibu Kondo alisema wao wana nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kwenye mechi ya leo kutokana na maandalizi mazuri waliyofanya.
"Hatuwaogopi Yanga na tumejipanga kuhakikisha tunaibuka na ushindi kwenye mchezo wa leo kama ilivyokuwa kwa Simba," alisema Kondo.
Villa Squad iliwashangaza watu mwaka huu pale ilipowafunga Simba bao 1-0 ukiwa ni moja ya ushindi wake wa nne katika mechi 19 ilizocheza msimu huu.
Nahodha wa Villa, Nsa Job atakuwa na kazi moja ya kuhakikisha anawaongoza wenzake kuifunga timu yake ya zamani ya Yanga ili kufufua matumaini yao ya kubaki Ligi Kuu.
Pamoja na kushikilia mkia, Villa imefanikiwa kufunga mabao 20 wastani wa bao moja kwa mechi huku nahodha wao Job akiwa amezifumania nyavu mara nane.
Ubora huo wa safu ya ushambuliaji wa Villa ni kitu ambacho kocha Kostadin Papic wa Yanga anapaswa kuutafakari na kuangalia upya ukuta wake ulioruhusu mabao 16 wavuni msimu huu.
Kurejea kwa kiungo Haruna Niyonzima katika mechi hii kumetoa faraja mpya kwa kocha Papic.
Niyonzima atakuwa na jukumu moja la kuwatengenezea nafasi washambuliaji wake Kenneth Asamoah na Davies Mwape na kuna shaka kwamba wataendelea kusababisha maafa kwa ngome ya Villa iliyoruhusu mabao 40.
Kwa mara nyingine Shirikisho la Soka Tanzania TFF, limemteua mwamuzi Oden Mbaga mwenye beji ya Fifa kuchezesha mechi ya Yanga katika kipindi cha siku nne.
Mwamuzi Mbaga ndiye aliyechezesha mechi ya Jumatano iliyopita wakati Yanga iliposhinda 1-0 dhidi ya Lyon.
Mechi nyingine ya leo itachezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, ambapo Coastal Union watakuwa wenyeji wa Oljoro JKT ya mkoani Arusha.
Ligi itaendelea tena kesho kwa mechi mbili wakati vinara wa ligi Simba watakapokuwa wageni wa Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati Azam watakuwa wenyeji wa Ruvu Shooting Stars kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam.
Simba na Azam zitaingia uwanjani kwa lengo moja la kupata ushindi na kuendelea kubaki katika nafasi mbili za juu.
Simba pia watautumia mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar kama sehemu ya maandalizi yao ya mechi ya Kombe la Shirikisho dhidi ya ES Setif ya Algeria utaofanyika wiki ijayo.
No comments:
Post a Comment