tuwasiliane

Friday, March 2, 2012

02 MARCH.Yanga: Jamani baridi inatuua Cairo



Michael Momburi, Cairo
BARIDI kali inayofikia nyuzi joto 16 inayoendelea jijini Cairo imewashangaza na kuwachosha wachezaji na viongozi wa Yanga wakisema,"jamani hii baridi hapa itatuua."

Wachezaji wa Yanga wakiwa wamevalia track suti zao za kawaida walikutana na hali hiyo jana asubuhi majira ya saa moja wakati walipowasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Cairo.

Ili kupambana na baridi hiyo baadhi ya wachezaji wa Yanga walijikuta wakijificha na ukuta au kukusanyika kwenye makundi mithiri ya 'vifaranga vya kuku' wakisubiri kutoka kuelekea kwenye hoteli ya Holiday Inn ya kiwango cha kawaida sana ambayo ipo mbele ya uwanja wa Zamalek hapa jijini Cairo.

Watanzania wanaoishi hapa Cairo wanadai baridi ni zaidi ya ile ya mkoani Iringa, haina upepo lakini ni kali kama ya barafu na inapenya kwenye mifupa jambo ambalo lilifanya baadhi ya wachezaji licha ya kuwa walivaa suti za klabu walikuwa wakitetemeka na kujificha ndani muda wote.

"Tuliwapa tahadhari Yanga mapema, tulitarajia kwamba wangeenda kuweka kambi mikoa yenye baridi, kabla ya kuja hapa,"alisikika akisema Mtanzania mmoja anayeishi hapa na kuona huruma jinsi wachezaji walivyokuwa wakihangaika kwa baridi kwani suti walizokuwa nazo ni nyepesi na hazikusaidia.

Kwa mujibu wa maofisa wa ubalozi wa Tanzania mjini
hapa, viongozi wa Yanga walipewa taarifa hizo kabla timu haijaondoka Dar es Salaam ili wajiandae kuja na vifaa kamili.

Kocha wa Yanga, Kostadin Papic alionyesha kushangazwa na vifaa duni walivyokuja navyo huku akishindwa kujua nini cha kufanya kukabiliana na hali hiyo tete.

"Yaani hata sielewi nitafanya nini wachezaji wazoee hii hali kwa vile ni tatizo kubwa na pia ni ngumu kuizoea hali kwa muda mfupi, tatizo lingine ni kwamba hata wachezaji vifaa walivyokuja navyo sio imara kukabiliana na hii hali ya baridi kali,"alisema Papic.

"Ni hali ngumu, lakini ngoja tufanye mazoezi leo (jana) jioni tuone itakuwaje, hii baridi ni kali sana,"alisema kocha huyo raia wa Serbia ambaye timu yake inacheza na Zamalek kwenye Uwanja wa Jeshi mjini hapa Jumamosi ambako baridi inategemewa kufika nyuzi 15.

Jana mchana mvua ilinyesha katika maeneo mbalimbali mjini hapa na kusababisha hali kuzidi kuchafuka huku wenyeji wakidai kwamba ni hali ambayo itaendelea mpaka mwezi Aprili kwani huanza Oktoba.

Siku ya jana wachezaji hao walishinda vyumbani na walitarajia kutoka majira ya saa 12 za hapa sawa na saa moja ya Tanzania kwa ajili ya mazoezi mepesi.

Yanga inahitaji ushindi au sare ya mabao 2-2 kuitoa Zamalek kwenye michuano hiyo na wachezaji wameonyesha morali mkubwa ingawa baadhi yao wameonekana kuwa na mtingo wa mawazo na muda mwingi wamekuwa wakijifikiria.

Wapinzani wao Zamalek wanashangilia kurejea kwa Ahmed Hossam ìMidoî aliyekuwa nje kwa miezi mwili na kiungo wao Mahmoud Abdul-Razek 'Shikabala', kwa ajili ya mchezo huo wa kesho.

Baada ya kuumia kwa Amr Zaki, Ahmed Gaafar yuko mashakani kutokana na kujiumiza goti mazoezini huku Razak Omotoyossi akiwa nyumbani kwao Benin safu ya ushambuliaji wa Zamalek imeyumba.

Omotoyossi aliyekuwa akiiongoza Benin kwenye mechi ya kufuzu kushiriki CAN 2013 dhidi ya Ethiopia juzi anaweza kuikosa mechi ya Yanga kama akishindwa kuwasili leo kambini.

Kocha Hassan Shehata atalazimika kumwanzisha Mido ambaye ndio kwanza amemaliza programu ya chakula kutokana na kuongezeka uzito na anaweza kuanza kwa mara ya kwanza tangu alipojiunga na klabu hiyo mwaka jana.

Zamalek itaingia kwenye mchezo huo wakiamini sare yao ya bao 1-1 waliyoipata ugenini itawatosha kufuzu.

No comments:

Post a Comment