tuwasiliane

Monday, February 27, 2012

27 FEB.SAMATA AZIDI KUONESHA CHECHE KWENYE LIGI YA DRC



MSHAMBULIAJI Mbwana Samata ameendelea kung'ara na TP Mazembe baada ya kuiongoza kupata ushindi wa mabao 4-1 kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya US Hyper Pasaro Kenya.

Samata alitemwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania na kocha Jan Poulsen kwa madai mchezaji huyo ameshindwa kuisaidia Taifa Stars katika mechi tatu zilizopita alizoichezea.

Tangu Poulsen alipotangaza kumwacha kwenye kikosi cha Stars tayari ameshafunga mabao matatu katika mechi mbili alizoichezea TP Mazembe.

Samata alifunga bao lake kwa ufundi mkubwa kwa kuwatoka mabeki wa US Hyper Pasaro na kupiga shuti lililomshinda kipa na kujaa wavuni.

TP Mazembe ikicheza mechi hiyo katika uwanja wake mpya ilipata bao la kwanza katika dakika ya 31 ambalo lilifungwa na Guy Lusadisu.

Mbwana Samata alifunga bao la pili kiufundi na hivyo TP Mazembe kwenda mapumziko ikiwa inaongoza kwa mabao 2-0.

Pia, katika mechi hiyo mshambuliaji Thomas Ulimwengu aliisumbua ngome ya US Kenya na alitoa pasi ya bao la nne la TP Mazembe lililofungwa na Luka Lungu.

Bao lingine la Mazembe lilifungwa na Eric Bokanga Kanteng katika dakika ya 51, wakati lile la kufutia machozi kwa US Kenya lilifungwa kwa faulo iliyopigwa na Didier Kalenga na kwenda moja kwa moja nyavuni.

Hata hivyo, kikosi cha Taifa Stars chini ya Poulsen kilikamilika jana baada ya kuwawasili kwa kiungo Nizar Khalfan tayari kwa mechi ya Jumatano dhidi Msumbiji.

Stars inajiandaa na mechi hiyo ya Kimataifa ya kuwania kufuzu kushiriki Fainali za Mataifa Afrika 2013, zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini, mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili, Poulsen alisema yuko katika maandalizi ya mwisho mwisho kuhakikisha wanafanya vizuri katika mechi na Msumbiji na ana matumaini makubwa baada ya kikosi hicho kukamilika.

''Tuko katika maandalizi na tumefarijika kwa wachezaji wote kuwasili kwa wakati kwa ajili ya mchezo huo,"alisema Poulsen.

Poulsen alimjumuisha Vicent Barnabas wa Mtibwa Sugar kwa lengo la kuziba pengo la Nizar kama angechelewa, hata hivyo ameahidi kutompunguza mchezaji yeyote.

''Hayo yalikuwa malengo yangu, hata hivyo Nizar amekuja, sitampunguza mchezaji yeyote kwa sababu wote tutawatumia,''alisisitiza kocha huyo

No comments:

Post a Comment