BAADHI ya walimu wapya wa shule za msingi walioripoti kazini katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida wanadaiwa kuwasilisha tiketi za nauli zenye utata hali ambayo halmashauri imelazimika kufanya uhakiki kabla ya kuwarejeshea nauli.
Ofisa Elimu wa Wilaya katika Halmashauri hiyo, Patrick Mwaluli, alisema kuwa walimu 147 walioripoti ni wale wa daraja la III A na kwamba wameshalipwa fedha zao za kujikimu isipokuwa nauli kutokana na utata uliojitokeza. Halmashauri imepangiwa walimu 170.
“Kwenye nauli hizi kuna utata mkubwa, kwa mfano wapo waliotoka Morogoro tiketi zao zinaonesha kuwa nauli ni Sh 40,000... waliotoka Dar es Salaam ambako ni mbali zaidi eti nauli ni Sh 28,000 tu. Ni dhahiri kuna tatizo, tunaendelea kuhakiki tiketi hizo,” alisema Mwaluli.
Alisema kuwa bado wana kazi ya kuangalia uhalali wa tiketi hizo kwa kulinganisha na gharama zilizoainishwa na Sumatra .
"Baada ya kujiridhisha, basi tutawarejeshea nauli zao haraka iwezekanavyo," alisema. Mwaluli alieleza kuwa kabla ya walimu hao wapya kuripoti, Halmashauri hiyo ilikuwa na walimu 1,654 wa shule za msingi kati ya mahitaji halisi ya walimu 2,403.
Alisema kuwa iwapo walimu wote 170 waliopangiwa kuanza kazi wataripoti, bado halmashauri hiyo itakuwa na upungufu wa walimu 578.
Ofisa Elimu huyo alitoa mwito kwa wananchi kuendelea kuboresha mazingira ya kufundishia, ikiwemo ujenzi wa nyumba za walimu kama njia mojawapo ya kuwavutia walimu kufanya kazi katika maeneo yao.
SOURCE HABARI LEO
No comments:
Post a Comment