
SIKU chache baada ya kampuni ya Vodacom kumaliza muda wake wa kudhamini mashindano ya Miss Tanzania, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), imeingia mkataba wa miaka mitatu kudhamini mashindano hayo.
Mashindano ya Miss Tanzania yamekuwa yakifanyika nchini kila mwaka kuanzia ngazi ya vitongoji hadi Taifa na TBL imedhamini mashindano hayo kwa jumla ya shilingi milioni 700.
Akizungumza jana mara baada ya kutiliana saini mkataba wa miaka mitatu, Meneja masoko wa TBL, Fimbo Butallah alisema Redds imekuwa ikishiriki katika mashindano hayo ya ulimbwende kwa miaka mingi kama mdhamini mwenza na kwamba msimu huu wameingia kama wadhamini wakuu.
"Sasa hivi mashindano hayo yatakuwa yakijulikana kama Redds Miss Tanzania na mkataba wetu utakuwa kila mwaka kwa miaka mitatu,"alisema Butallah.
Naye Meneja wa Redds, Victoria Kimaro alisema udhamini huo utaanzia ngazi ya vitongoji hadi Taifa na kwamba wataliboresha zaidi shindano hilo msimu huu ili kuleta msisimko kwa mashabiki na wadau wa tasnia hiyo.
Akizungumzia tukio hilo muhimu mratibu wa Miss Tanzania, Hashim Lundenga aliishukuru Redds kwa mkataba wao ambao umewahakikishia udhamini wa miaka mitatu.
"Tunawapongeza kwa kuwa mstari wa mbele katika kuendeleza tasnia ya urembo hapa nchini, tumekuwa bega kwa bega kwa miaka kadhaa sasa na haiwezekani ukazungumzia tasnia ya urembo hapa nchini bila ya kutaja Redd's Original,"alisema Lundenga.
TBL kupitia vinywaji vyake imekuwa ikidhamini mashindano hayo mara kwa mara ikiwamo Plisner Ice miaka ya nyuma.
No comments:
Post a Comment