tuwasiliane

Thursday, February 2, 2012

02 FEB. Makala amkaanga Sumaye Mjengoni!


Jana mjengoni (Bungeni) ilikuwa patashika pale Mbunge wa Mvomero, Amos Makalla (CCM), alipomtuhumu Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, kwamba amekwapua ekari 326 za shamba la ushirika la wilayani Mvomero lililopaswa kugawanywa kwa wanakijiji wa Mvomero, mkoani Morogoro.

Kutokana na hali hiyo, mbunge huyo alihoji utaratibu uliotumiwa na serikali kumuuzia Sumaye shamba hilo badala ya kuwapa wananchi kipaumbele.

Makalla aliitaka serikali itoe tamko kuhusu shamba hilo kwakuwa Rais JK wakati wa kampeni zake mwaka 2010, aliwahi kuahidi kushughulikia kero hiyo.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Goodluck Ole-Medeye, alisema kuwa shamba hilo lenye hati namba 21919, lililoko katika Kijiji cha Mvomero, Wilaya ya Mvomero, linamilikiwa na mke wa Sumaye, Esther Sumaye kihalali.

Alisema kabla ya shamba hilo kumilikiwa na Esther Sumaye, lilikuwa likimilikiwa na Onasaa Waryaeli Kisanga na Mesaki Josiah Ndanshau, wakitumia jina la Mvomero River Farm Limited kwa hati namba 211919.

“Aidha, tarehe 27, Novemba 2001, wamiliki hao walimuuzia mke wa Sumaye 'Esther Sumaye' shamba hilo na baada ya kukamilisha taratibu zote za kisheria ikiwa ni pamoja na kulipa ushuru kwa serikali, uhamishwaji wa miliki ulikamilishwa mwaka 2002 kwa mujibu wa kifungu cha 61 cha sheria ya ardhi namba 4 ya mwaka 1999,” alisema naibu waziri.

Kwa kuwa Esther Sumaye ana miliki shamba hilo kihalali na kuliendeleza kwa kuzingatia masharti ya hatimiliki, waziri alisema serikali inaheshimu haki zake na kwenye ibara ya 24 (1) na (2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.

No comments:

Post a Comment