tuwasiliane

Sunday, January 29, 2012

29 JAN.TWIGA STARS VITANI LEO


TIMU ya soka ya Taifa ya wanawake Twiga Stars leo itaumana na wenzake wa Namibia katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa Afrika kwa Wanawake kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Fainali za michuano hiyo zimepangwa kufanyika Zimbabwe mwishoni mwa mwaka huu.
Twiga inaingia uwanjani ikiwa kifua mbele baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika mechi ya awali iliyochezwa wiki mbili zilizopita mjini Windhoek.

Akizungumzia mchezo huo wa leo Nahodha wa timu hiyo Sophia Mwasikili alisema kuwa wachezaji wake wapo katika hali nzuri kiafya tayari kuikabili Namibia. Alisema kuwa kupitia Kocha wa timu yao Boniface Mkwasa wameweza kujifunza mbinu mpya za kuwakabili wapinzani wao.

“Katika mchezo wetu wa Namibia wachezaji walishindwa kutumia nafasi nyingi na kujikuta tukikosa mabao mengi lakini mechi ya kesho (leo) tumejipanga vizuri”.

Aliongeza kuwa wamejifunza mbinu za ukabaji na ushambuliaji ambazo watazitumia katika kuikabili timu ya Namibia.

“Ni kwamba kwa sasa tunaona kuwa kesho “ leo” ushindi upo mbele yetu kwa asilimia mia moja kwa kuwa tumeongeza mbinu mbadala za kuishinda timu ya Namibia” alisema. Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya Namibia Klaus Staerk alisema kuwa timu yake imekuja Tanzania kupata ushindi na sio kukamilisha ratiba.

Alisema anatambua kuwa Twiga ni timu nzuri na yenye uwezo na ndio maana iliweza kuwafunga nchini kwao (Namibia) na kuongeza kwa sasa wameshagundua mbinu mpya za kukabiliana nao.

Alisema kuwa timu yake inajitahidi kuyazoea mazingira ya hali ya hewa ya hapa nchini ambayo ni ya joto ikilinganishwa na Namibia ambapo kuna baridi. Pia aliongeza kuwa kocha wa timu yao anaumwa tumbo lakini hata hivyo wanatarajia kuwa atapona na kukisimamia vema kikosi chake hicho.

“Tumekuja hapa Tanzania kushinda licha ya kuwa tunaona kuwa changamoto kubwa iliyopo mbele yetu ni hii hali ya hewa kuwa ni joto huku kwetu Namibia tumezoea baridi, lakini hata hivyo tutajitaidi kufanya vema” alisema Stark.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Angetile Osiah alisema kuwa TFF itaendelea na kampeni ya kuchangisha fedha za kusaidia timu hiyo.

Alisema kuwa Bohari ya Madawa imewapatia Sh milioni 10 na pia kuna wadau wengine mbalimbali wameahidi kuwasaidia zaidi. Mwisho./fm

No comments:

Post a Comment