
MAMIA ya wakulima kutoka vijiji vya Kata ya Msowero kikiwemo cha Mambegwa katika Tarafa ya Magole, wilayani Kilosa juzi walifunga barabara kuu ya Kilosa – Dumila na kusababisha usumbufu.
Walifunga barabara hiyo kwa saa 12 wakishinikiza uongozi wa Serikali ya wilaya hiyo kutatua mgogoro wa mipaka kati ya Kijiji chao cha Mambegwa na Mabwelebwele .
Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Halima Dendego alilazimika kufika eneo la tukio ili kuzungumza na wananchi hao waliokuwa wamejawa na hasira huku wakiwa wameshika mabango.
Hata hivyo, kutokana na hali hiyo, Askari Polisi wa Kituo Kikuu cha Wilaya ya Kilosa na Dumila wakiwa na dhana za kutuliza fujo waliwasili eneo la tukio na kuwataka wananchi hao kuondoa mawe makubwa na magogo waliyoziba pande mbili za daraja la Mto Msowero linalotenganisha Kilosa na Dumila.
Pamoja na kukataa huko, polisi walitumia busara ya kutotumia nguvu ya kuwatawanya kwa mabomu na badala yake walimsubiri Mkuu wa Wilaya kama madai ya wananchi hao ili kupata majawabu muafaka.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mambegwa ambao wamekuwa na mgogoro wa mipaka na kijiji chenye wafugaji wengi cha Mabwerebwere, Ramadhan Munuo, Shomari Mkopi na Hamis Msabaha, kwa nyakati tofauti walidai kuwa wakulima wamekuwa wakinyanyaswa na wafugaji kutokana na uduni wa vipato vyao.
Hata hivyo, alidai kuwa pamoja na kushinda kesi ya msingi mwaka 2010 katika Mahakama Kuu kitengo cha Ardhi kuhalalisha kuwa Kijiji cha Mambegwa ni cha wakulima, baadhi ya wafugaji walienda kukata rufaa Mahakama Kuu na tangu hapo kesi hiyo haijasikilizwa na kutolewa maamuzi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Dendego, alisema tatizo kubwa lililipo ni Kijiji cha Mabwegele cha wafugaji kuzungukwa na vijiji vya wakulima na kukosekana maamuzi ya kijiji mama.
Hivyo aliwaomba wananchi hao na jamii ya wafugaji waliopo katika mgogoro huo, kuondoa kesi ya rufaa iliyofunguliwa Mahakama Kuu ama iharakishwe kutolewa maamuzi ili Serikali ya Wilaya iweze kuanza kupima mipaka ya vijiji hivyo ili kuondoa migogoro kama wananchi wanavyohitaji.
No comments:
Post a Comment