WAANDAAJI wa mashindano ya Kombe la Mapinduzi wametoa ratiba ya michuano hiyo, inayoonesha kuwa timu za Yanga na Azam za jijini Dar es Salaam zimewekwa kundi moja.
Kulingana na ratiba hiyo iliyotolewa jana kwa waandishi wa habari na msemaji wa Kamati ya
Kombe la Mapinduzi, Farouk Karim, Yanga itakuwa Kundi B na Azam, Mafunzo ya Unguja na Kikwajuni ya Pemba.
Kwa mujibu wa Farouk Kundi A lina timu ya Simba ya Dar es Salaam ambao ni mabingwa watetezi, Miembeni United na KMKM za Unguja pamoja na Jamhuri ya Pemba.
Ratiba inaonesha kuwa mashindano hayo yataanza Januari 2 mwakani, ambapo jioni Azam
itacheza na Kikwajuni na usiku Yanga itacheza na Mafunzo, mechi zote zikiwa kwenye Uwanja wa Amani.
Farouk alisema kuwa Januari 3 Miembeni United itacheza na KMKM na usiku Simba itacheza
na Jamhuri kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.
Awali jana, mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Kombe la Mapinduzi, ambaye hakutaka kutajwa
jina lake kwa madai sio msemaji alisema kwamba Yanga ilikuwa bado haijathibitisha ushiriki
wake.
Alisema kutokana na hali hiyo Kamati ya Kombe la Mapinduzi ilikuwa kwenye wakati mgumu
wakati wa kupanga ratiba, ingawa baadaye walikubaliana waiweke.
“Haya si mashindano ya mtu binafsi ni ya taifa na kama haitashiriki tutasema kuwa wametudharau,” alisema mjumbe huyo.
Alieleza kuwa kama Yanga haitashiriki ni vyema ingewaeleza mapema ili waweze kutafuta timu
mbadala badala ya kuamua kukaa kimya mpaka sasa.
Lakini akizungumza jana, Ofisa Habari wa Yanga, Luios Sendeu alisema Yanga itashiriki
mashindano hayo kama walivyopanga na kueleza kuwa Kamati ya Ufundi ya Yanga inalishughulikia suala hilo kwa ukamilifu zaidi.
“Tutacheza hakuna wasiwasi… Yanga haiwezi kukimbia kucheza,” alisema Sendeu.
Akizungumza baadaye jana Farouk alisema Yanga itashiriki mashindano hayo na ndiyo
sababu wameiweka kwenye ratiba.
No comments:
Post a Comment