tuwasiliane

Sunday, December 25, 2011

25 DEC.SETTLE SOUNDERS YAMPOTEZEA NGASA


HATIMA ya mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars na klabu ya Azam FC, Mrisho Ngasa kujiunga na timu ya Seattle Sounders ya Marekani ipo mashakani kutokana na kutoeleweka kinachoendelea sasa baada ya kukatika kwa mawasiliano.

Akizungumza na Mwandishi wa blogu hii, Katibu Mkuu wa timu ya Azam FC, Nassoro Idrissa alisema pamoja na Ngassa kufanya majaribio na kuchezea mechi ya kihistoria dhidi ya Manchester United, mpaka sasa hakuna mawasiliano yoyote.

Idrissa alisema baada ya Ngassa kurejea nchini na kupewa ahadi ya kurudi tena Marekani, hawajapata taarifa tena kama.

Alisema kwa sasa Seattle Sounders inaendelea na usajili wa wachezaji wake kwa ajili ya msimu ujao na walitarajia kuona Ngassa anakwenda huko ili kukamilisha zoezi hilo au kwa majaribio kabla ya hatua nyingine.

“Kwa sasa hatufahamu lolote kuhusiana na hatima ya Ngassa, hakuna mawasiliano yoyote na kwa vile Ngassa ni mchezaji wetu, basi ataendelea kuichezea timu yetu kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara na mashindano mengine,” alisema Idrissa.

Alisema kuwa bado wana matarajio mchezaji wao kuichezea timu hiyo au nyingine kwani ni miongoni mwa wachezaji wenye vipaji na hazina kubwa kwa timu yao na timu ya Taifa.

“Sisi halituumizi na si tatizo kwetu, kwanza hatujatumia gharama yoyote katika mchakato mzima. Lakini nisema kwamba hatukauwa na kipingamizi, tutajadiliana nao kuwaeleza matakwa yetu, ikishindikana ataendelea kuwa Azam,” alisema.

Mratibu wa majaribio hayo, Rahim Kangezi alisema kuwa anasubiri mawasiliano kutoka kwa timu hiyo japo si kiongozi wa Azam FC.

“Mimi ni kiongozi wa African Lyon, sitahusika na makubaliano yoyote kuhusiana na usajili wa Ngassa, sijui kimekwama nini, ila najua usajili bado mpaka Machi mwakani,” alisema Kangezi.

Alisema kuwa endapo Seattle Sounders watamwita Ngassa kwa majaribio, itabidi apitie utaratibu wa kimataifa wa kupimwa afya yake kabla ya kusaini.

No comments:

Post a Comment