
BAADA ya kutoweka kwa kipindi kirefu, hatimaye beki wa kati wa Simba, Kelvin Yondani, amerejea rasmi kundini kisha akakutana uso kwa uso na kocha wake mpya, Mserbia Milovan Cirkovic ‘Profesa Chico’.
Yondani alitimka kwenye kambi ya timu hiyo tangu Septemba, mwaka huu, wakati Simba ilipokwenda Kanda ya Ziwa kucheza dhidi ya Toto na Kagera chini ya aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Moses Basena.
Tangu wakati huo, Yondani hakuonekana mpaka jana (Alhamisi) alipojitokeza kwenye mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Kinesi jijini Dar es Salaam, yaliyosimamiwa na Profesa Chico na msaidizi wake Amatre Richard, raia wa Uganda.
Mazoezi hayo yalifanyika kwa dakika 23 tu kutokana na mvua kali iliyosababisha uwanja kutokuwa na hali nzuri. MWANDISHI WETU ALIPOMUULIZA Yondani kilichotokea akatoweka kambini alisema: “Nilikuwa na matatizo ya kifamilia na ni vigumu kuyaeleza matatizo binafsi kwa jamii.
“Lakini yameisha na nimerejea Simba kwa ajili ya kucheza mpira na siyo kingine, nimekaa nje kwa muda mrefu, naamini siku hizi zilizobaki zitatosha kwa maandalizi kabla ya ligi kuanza.”
Naye Katibu Mkuu wa Simba, Evodius Mtawala alisema: “Tumempokea mchezaji wetu leo (jana) baada ya kumaliza matatizo ya kifamilia. Kilichomsababishia kuondoka kambini ni matatizo ya kifamilia ambayo ni siri na viongozi tu ndiyo tulioelezwa.”
Katika hatua nyingine, Profesa Chico amelalamikia Uwanja wa Kinesi ambao wanautumia kwa ajili ya mazoezi kutokana na kutokidhi kiwango cha kutumiwa na klabu kubwa kama ya Simba.
No comments:
Post a Comment