
Uongozi wa klabu ya Mamelodi Sundowns inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini imevutiwa na kiwango cha mshambuliaji nyota wa timu ya soka ya taifa ya vijana ya umri chini ya miaka 20 ya Tanzania, Ngorongoro Hereos, Simon Msuva.
Msuva aling'ara katika mashindano ya COSAFA yanayoendelea jijini hapa ambapo aliifungia timu yake magoli matano na kutengeneza nafasi mbalimbali katika mechi tatu za hatua ya makundi. Licha ya kutopoteza mechi hata moja, Ngorongoro iliyoshinda mechi moja na kutoka sare mbili, ilitarajiwa kutua jijini Dar es Salaam saa 10:00 alfajiri ya leo.
Akizungumza na WAANDISHI WA HABARI jana, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Mamelodi Sundowns, Ernest Ntawali, alisema kwamba klabu yake inamuhitaji mshambuliaji huyo na endapo uongozi wa Ngorongoro Hereos, utakuwa tayari kumruhusu wanataka wamchukue na kwenda nae Johannesburg, Afrika Kusini kwa ajili ya kuanza majaribio.
Ntawali ambaye yuko jijini hapa kwa ajili ya kuangalia wachezaji alisema kwamba pia amevutiwa na mshambuliaji mwingine wa Ngorongoro Heroes, Edward Christopher, ambaye naye ana nafasi ya kuanza kusajiliwa kwenye timu ya vijana ya klabu hiyo.
"Nimevutiwa na mchezaji aliyevaa namba 11 (Msuva) sana, ni mwenye kipaji na ndiye mchezaji aliyeng'ara katika mechi dhidi ya Zambia, pia namba 17 (Edward) ni mzuri, kama mambo yanaenda vizuri, tutawachukua kwenda Johannesburg waanze majaribio," alisema Ntawali ambaye aliichezea Mamelodi Sundowns kwa zaidi ya miaka 15 pamoja na timu yake ya taifa ya Malawi.
Aliongeza kuwa mashindano haya yanayoendelea ni mazuri kwa klabu kusaka vipaji kwa sababu wachezaji wengi ni vijana na wamepata misingi ya soka na kinachofuata ni kuwaendeleza na kuungana na mfumo wa timu inavyocheza tofauti na kusajili wachezaji wenye umri mkubwa.
"Ukipata wachezaji wanne au watano hapa, ujue una uhakika wa kuwa na timu bora ndani ya miaka miwili, bado ni vijana na wana ari ya kupata mafanikio, akili yao sasa ni soka, jambo ambalo litaisaidia timu kusonga mbele," aliongeza nyota huyo.
Mbali na kiongozi huyo wa Mamelodi Sundowns, pia makocha mbalimbali walioko hapa walimtaja Msuva kuwa ni hatari na Tanzania inatakiwa kumuendeleza ili iweze kufaidika na kipaji cha mchezaji huyo.
Kocha Mkuu wa timu ya vijana ya Zambia, Keegan Mumba, aliwaambia waandishi kwamba, Msuva, aliisumbua ngome yake ya ulinzi muda wote wa mchezo na hakuamini kiwango kilichoonyeshwa na timu ya Ngorongoro Heroes.
Mumba alisema kwamba mchezaji huyo aliisaidia timu yake kuisumbua Zambia tofauti na walivyoifikiria mechi hiyo kabla ya kuanza kwa mchezo.
Kocha wa zamani wa Yanga ya Tanzania, Jack Chamangwana, ambaye sasa anaifundisha timu ya vijana ya Malawi, alisema kwamba Tanzania imebadilika na wachezaji wake vijana wana uwezo mkubwa hivyo wanapaswa kuendelezwa ili kuacha tabia ya kusajili wachezaji wa nje ambao uwezo wao si mkubwa.
No comments:
Post a Comment