
NYOTA wa kimataifa wanaocheza Simba wanatarajiwa kutua nchini kesho tayari kwa mchezo wao dhidi ya Asante Kotoko ya Ghana utakaofanyika Jumapili hii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wachezaji hao wa kulipwa watakaowasili leo ni pamoja na Mzambia Felix Sunzu na Gervais Kago wa Jamhuri ya Afrika Katu na kuungana na wenzao tayari kwa mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa wenye lengo la kusherehekea miaka 50 ya Uhuru.
Afisa habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema tayari timu hiyo imeanza mazoezi yake kwenye Uwanja wa Kinesi na wachezaji wote wamejumuika isipokuwa wale wanaotumikia timu zao za taifa kwenye Michuano ya Chalenji itakayofikia tamati kesho.
Kamwaga alisema kimsingi pambano hilo litakua sehemu ya maandalizi yao katika mzunguko wa pili wa Ligi Kuu pamoja na kuwatambulisha nyota wao wapya waliowasajili katika usajili wa dirisha dogo.
"Tunaendelea na maandalizi yetu vizuri licha ya wapinzani wetu Yanga kukataa kujumuika na sisi, lakini hakuna kilichoharibika kwani tayari sisi kama Simba tumekubali kucheza na tunaamini mchezo huu utakua sehemu ya maandalizi yetu,"alisema Kamwaga.
Wakati huo huo; Kikosi cha wachezaji 20, viongozi 10 na waandishi wa Habari 10 kinawasili nchini leo kutoka Ghana, tayari kwa mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Mabingwa wa Ngao ya Jamii, Simba SC.
Asante Kotoko watawasili asubuhi ya leo wanatarajiwa kushiriki katika maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru kwenye uwanja wa uhuru jijini Dar es Salaam kabla ya kesho kutwa kushuka dimbani kuvaana na Simba.
Mkurugenzi wa Future Century waandaaji wa mchezo huo, Alberto Albano alisema kuwa Asante Kotoko wanakuja nchini kama ishara ya kumuenzi mhasisi wa Tanzania Hayati baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa rafiki mkubwa wa rais wa kwanza wa nchini hiyo Kwame Nkurumah.
Albano alisema kuwa kabla ya mechi hiyo kutakuwa na burudani mbalimbali kama ngoma, bendi na burudani nyingine nyingi kuanzia saa nne asubuhi ambapo milango itafunguliwa uwanjani hapo kabla ya jioni mabingwa hao kutumishiana msuli.
Awali mechi hiyo ilipangwa kuwakutanisha wachezaji wa Simba na Yanga ambao wangeunda timu ya kombaini kucheza na Asante Kotoko licha ya kwamba Yanga iliamua kujitoa dakika za mwisho kuungana na wapinzani wao wa jadi.
No comments:
Post a Comment