
Mshambuliaji Mussa Hassan Mgosi wa klabu ya DC Motema Pembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameitwa kuungana na nyota wengine 28 waliotangazwa juzi kuunda kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Bara’Kilimanjaro Stars’ kitakachoanza kujifua ufukweni mwa bahari ya Hindi leo asubuhi kujiandaa na michuano ya Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Chalenji) itakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Novemba 25.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, kocha msaidizi wa Kilimanjaro Stars, Jmahuri Kihwelu ‘Julio’ alisema kuwa wameamua kumuita Mgosi ili kukiongezea makali kikosi hicho kwani taarifa walizopata kuhusiana na nyota huyo wa zamani wa ‘Wekundu wa Msimbazi’, Simba zinaonyesha kuwa yuko katika kiwango cha juu cha upachikaji mabao.
Julio alisema kuwa takwimu za Mgosi nchini Kongo zinaonyesha kuwa amepachika mabao sita katika mechi nane alizocheza, kiwango ambacho ni cha juu na hivyo wanaamini kuwa ataisaidia Stars kutetea ubingwa wa Chalenji.
“Tumeita wachezaji wengi ili mwishowe tupate 20 watakaotetea ubingwa wetu,” alisema Julio.
Akieleza zaidi, Julio alisema kuwa kikosi chao ambacho sasa kina wachezaji 29 kitaanza kujifua Coco Beach kwa saa mbili ili kuanza kujenga stamina kabla ya kupata mbinu za kiufundi.
Stars iliyotwaa kombe la Chalenji mwaka jana kwa kuwafunga waalikwa Ivory Coast bao 1-0 katika mecghi yao kali ya fainali iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, itaanza kutetea taji lake kwa kucheza Novemba 26 dhidi ya Rwanda katika mechi yao ya ufunguzi wa Kundi A. Wapinzani wengine katika kundi lao ni Djibout na Namibia walioalikwa baada ya Eritrea kujitoa.
Awali, nyota 28 waliotangazwa na Julio juzi kwa niaba ya kocha mkuu Charles Boniface Mkwasa ni makipa Juma Kaseja (Simba), Shaabn Kado (Yanga) na Deo Munishi ‘Dida’ (Mtibwa), mabeki wa pembeni ni Shomari Kapombe na Juma Jabu (Simba), Godfrey Taita (Yanga) na Paul Ngelema (Ruvu Shooting).
Mabeki wa kati ni Juma Nyoso (Simba), Said Murad (Azam), Erasto Nyoni (Azam) na Salum Telela (Moro United).
Viungo walioitwa Kili Stars ni Shaabn Nditi (Mtibwa), Ibrahim Mwaipopo (Azam), Nurdin Bakari (Yanga), Mwinyi Kazimoto na Haruna Moshi ‘Boban’ (Simba), Ramadhani Chombo ‘Redondo’ (Azam), Rashid Yusuf (Coastal), Jimmy Shogi (JKT Ruvu), Nizar Khalfan wa Vancouver Whitecaps ya Canada.
Mohamed Soud wa Toto African.
Washambuliaji ni Mrisho Ngasa (Azam), Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe ya Kongo DR), Gaudence Mwaikimba (Moro United), John Bocco (Azam), Hussein Javu (Mtibwa) na Daniel Reuben (Coastal).
No comments:
Post a Comment