tuwasiliane

Thursday, May 24, 2012

24 MAY. ulimwengu aumia mazoezini stars


TIMU ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' imepata pigo jingine baada ya mshambuliaji wake Thomas Ulimwengu naye kuumia kifundo cha mguu.
Kuumia kwa Ulimwengu anayekipga katika klabu ya TP Mazembe ya Jmahuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kunafa timu hiyo kufikisha majeruhi wawili ambapo jana, kiungo wake Nurdin Bakari alichanika nyama za paja hali itakayomlazimu kukaa nje ya dimba kwa siku saba.

Daktari wa Stars, Mwanandi Mwankemwa amekiambia Chanzo chetu Ulimwengu alipata maumivu hayo wakati wa mazoezi ya timu hiyo kwenye uwanja wa Karume, jijini Dar es Salaam.

Alisema kutokana na maumivu hayo, Ulimwengu naye ataukjosa mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Malawi utakaopigwa jumamosi kwenye dimba la Taifa jijini Dar es Salaam.

Stars inayonolewa na Mdenmark Kim Poulsen akisaidiwa na Mzalendo Sylvestre Marsh imepiga kambi kwenye hoteli ya Tansoma jijini Dar es Salaam ikijiandaa mechi yake ya mchujo kufuzu Kombe la Dunia hatua ya makundi Kanda ya Afrika dhidi ya Ivory Coast itakayopigwa Abidjan Juni 2 mwaka huu.

24 MAY. HABARI PICHA


Rais Jakaya Kikwete akimsaidia Waziri asiye na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya kushuka kwenye ngazi za Ikulu, Dar es Salaam, baada ya kuapishwa rasmi jana kushika wadhifa huo. (Picha na Freddy Maro).

24 MAY.Shibuda sasa amvaa Dk Slaa,adai kuwatumia Bavicha


MSUGUANO wa vijana wa Chadema (Bavicha) na Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki , John Shibuda, umezidi kuongeza joto la kisiasa ndani ya chama hicho baada ya mbunge huyo kumrushia kombora Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa, akisema ndiye anayewatumia vijana hao kumhujumu.

Tayari Shibuda ameigawa Bavicha baada ya Mwenyekiti wake, John Heche kupingana hadharani na makamu wake, Juliana Shonza kuhusu msimamo wa baraza hilo dhidi ya hatua ya mbunge huyo kutangaza dhamira ya kuwania urais mwaka 2015 ndani ya Nec ya CCM na kumwomba Mwenyekiti wa chama hicho tawala, Rais Jakaya Kikwete awe kampeni meneja wake.

Wakati kauli zake hizo ndani ya Nec ya CCM zikitarajiwa kumweka katika hatari ya kufukuzwa ndani ya Chadema kipindi hiki ambacho amekuwa katika uangalizi maalum, Shibuda jana aliliambia Mwananchi kwamba, yuko tayari kwa lolote na wakati wowote tena kwa asilimia 100.

Shibuda alifafanua kwamba anatuhumiwa kukihujumu chama huku akiwa hajawahi kukiuka maagizo yoyote ya Kamati Kuu ndani ya Chadema , lakini amebaini kuna baadhi ya watu wanatumiwa na viongozi wa juu wa chama hicho akiwamo Dk Slaa kwa lengo la kumfanyia fitina na hujuma.

Alisema kitendo cha Dk Slaa kukalia kimya shutuma zinazoelekezwa kwake na vijana hao wa Chadema kinampa fursa ya kuamini kwamba vigogo wa chama hicho wako nyuma yao na kumtaka sasa Dk Slaa aeleza hadharani uovu wake huo ili Watanzania wafahamu ukweli kuhusu sakata hilo.

"Mimi sina kosa lolote ila ninachofikiria ni kwamba Bavicha wanatumiwa na viongozi wa juu wa Chama ili kutaka kuniharibia lakini cha msingi ni vyema Katibu Mkuu wetu (Dk Slaa), akaweka hadharani maovu yangu ili Watanzania wajue makosa yangu ni yapi," alisema Shibuda na kuongeza:
"Ni wakati wa Chadema kupitia viongozi wake wakuu kueleza ubora wake wa kuwaongoza wananchi uko wapi kwani kama mtu anatangaza nia na kuonekana ameenda kinyume, sidhani kama kuna uongozi thabiti."

Kitisho cha kufukuzwa
Akizungumzia kitisho cha kuweza kufukuzwa Chadema, Shibuda alisema kwa sasa yupo tayari kwa asilimia 100 kupokea jambo lolote litakalotokea dhidi yake ndani ya chama hicho na kwamba kinachotakiwa ni kuonyeshwa makosa yake.

"Kwa asilimia 100, kutoka moyoni nasema nipo tayari kwa lolote litakalotokea kwangu ndani ya Chadema, kwani mimi natambua wazi sina kosa nililolifanya na kama nina makosa basi yaanikwe hadharani ili wananchi nao watambue," alisema.

Akizungumzia kupewa barua ya karipio kali, Shibuda alisema kwamba, hata siku moja hajawahi kupewa barua yoyote ya karipio kali na hafahamu chochote juu ya suala hilo.

"Sikiliza ndugu mwandishi, mimi sijawahi kupewa barua yoyote ya karipio kali na sifahamu chochote juu ya suala hilo labda hao walionipa barua hiyo wangeeleza lini walinipa," alisema.

Kauli ya Dk Slaa/ Heche
Akizungumzia tuhuma hizo za Shibuda, Dk Slaa alisema asingependa kuingizwa katika mjadala huo kwani hajawahi kumzungumzia Mbunge huyo kuhusu jambo lolote wakati wowote tangu mjadala wake na Bavicha ulipoanza.

Alisema haoni suala la Shibuda kama ni jambo la kuzungumzia kwa sasa kwani halina msingi na kuna mambo mengi ya kujadili ili kuliwezesha taifa kupambana na umasikini.

"Mimi nisingependa kuhusishwa na suala la Shibuda kwani sijawahi kuzungumza chochote kumhusu yeye na kwamba, nina mambo mengi ya kuangalia na sio Shibuda," alisema Dk Slaa na kuongeza:
"Sipendi kuzungumzia kauli za watu hata kidogo kwani tunakazi kubwa ya kupambana na kuwakomboa wananchi kutoka katika umasikini."

Heche, akizungumzia tuhuma hizo kwamba Bavicha inatumiwa kumhujumu Shibuda, alisema hawezi kuzungumzia suala la Shibuda sasa kwa kuwa tayari kuna vikao vimeanza kukaa kulijadili.
Alisema baada ya kukamilika kwa vikao vya Kamati tendaji ya Bavicha, watatoa majibu sahihi yanayohusu masula mbalimbali ya vijana, lakini pia watatoa ufafanuzi na msimamo wao kuhusu Shibuda.
“Tuna vikao ambavyo vinaanza kesho (leo) na baada ya kumalizika ndipo tunaweza kutoa ufafanuzi kuhusu mambo yote tutakayojadili ikiwa ni pamoja na msimamao wetu kuhusu Shibuda,” alisema Heche.

Matukio yake
Hi ni mara ya tatu kwa Shibuda kuingia katika mgogoro wa ndani ya chama kwani, mara ya kwanza aliwahi kukiuka msimamo wa wabunge wa Chadema kutoka nje ya ukumbi wa bunge kwa kupinga matokeo yaliyompa Kikwete Urais badala yake usiku alihudhuria dhifa maalumu Ikulu ndogo Chamwino baada ya mkuu huyo wa nchi kuzindua Bunge la kumi.

Shibuda pia aliwahi kuingia katika mgogoro na chama hicho kutokana na msimamo wake wa kuendelea kupokea posho za bunge na kutaka ziongezwe hadi kufika Sh500,000, akiziita "ujira wa mwiha," huku akirusha vijembe kwa baadhi ya wabunge wenzake akisema ni wafanyabiashara siyo wabunge jamii.
Matukio hayo yalimfanya aundiwe Kamati Maalumu chini ya Profesa Abdalla Safari kwa lengo la kuangalia nyendo zake na matokeo yake, ni kuwa chini ya uangalizi maalum ndani ya miaka miwili kuanzia sasa vinginevyo CC imfukuze lakini, ameibua mjadala mwingine wakati hata mwaka huo wa uangalizi maalumu haujakamilika.

Katika sakata hilo la sasa tayari kumeibuka mvutano ndani ya Bavicha baada ya Shonza kupinga tamko la Heche ambapo Mei 20, aliitisha mkutano na waandishi wa habari na kusema, “Naomba ifahamike kwamba tamko alilolitoa Heche siyo la

Baraza, bali ni lake kama Heche. Alipokuwa akitoa tamko hilo hakukuwa na kikao chochote cha Baraza cha viongozi wa kitaifa wala Sekretarieti ya Baraza la Vijana la Chadema ili kulijadili suala hili kwa kina bali, alitumia mwamvuli wa vijana kuhalalisha hoja yake.”

Hata hivyo, siku hiyo ya jioni Heche naye alitoa taarifa kwa umma akisema, “Nimejulishwa kuwa Makamu wangu (Shonza), leo (Mei 20) amezungumza na vyombo vya habari na kukanusha taarifa niliyotoa kwa niaba ya Bavicha.

Itambulike kuwa majukumu na mamlaka ya mwenyekiti na kiongozi mwingine yeyote wa Baraza yanabainishwa na Kanuni za Baraza letu kifungu 5.4.1, ambayo mwenyekiti ndiye msemaji mkuu wa Baraza na pia ndiye kiongozi mkuu wa Baraza katika ngazi husika.”

24 MAY.Mwalala, Shiboli watemwa Coastal


TIMU ya soka ya Coastal Union ya Tanga imewaacha wachezaji wake tisa wakiwemo Ally Ahmed ‘Shiboli’, Benard Mwalala na Ramadhan Wasso.

Pia timu hiyo ipo mbioni kumsajili kiungo wa zamani wa Simba ya Dar es Salaam, Mkenya Jerry Santo kwa nia ya kuimarisha kikosi chake kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.

Akizungumza na gazeti hili, Katibu Mkuu wa Coastal Union, Kassim El Siag alisema jana kuwa wachezaji hao tisa wapo huru kujiunga na timu nyingine yoyote na kuwataja kuwa ni Mwalala, Samueli Temi, Shiboli, Wasso, Enock John, Laurent Mugia, Bakari Mohamed, Daudi Changula na Francis Busungu.

Katibu huyo alisema moja ya sababu za kuchukua uamuzi huo ni kutokana na kushuka kwa viwango vyao vya uchezaji na kwamba wana matumaini makubwa timu yao mwakani itakuwa moto wa kuotea mbali.

Alisema Kamati ya Usajili ya Coastal Union inaendelea na harakati za kufanya usajili wa nguvu kuhakikisha wanafanya vizuri zaidi msimu ujao.

Wakati huohuo, Coastal ipo mbioni kumsajili kiungo Mkenya Jerry Santo, ambapo kwa mujibu wa Ofisa Habari wa klabu hiyo, Edo Kumwembe mazungumzo yanaendelea kuhusiana na kiungo huyo.

“Tuko kwenye usajili sasa hivi, tayari tumeishawanasa wachezaji wawili na sasa tuko katika hatu ya mwisho na Jerry Sant,” alisema Edo.

Aliwataja wachezaji ambao wamewasajili kuwa ni Nsa Job kutoka Villa Squad na kiungo Sudy Mohmed wa Toto Africans ya Mwanza.

24 MAY. SIMBA KUTANGAZA WALIOTEMWA SOON


WAKATI mabingwa wa Soka Tanzania bara, Simba SC wakimuongezea mkataba kocha mkuu wa timu hiyo, Milovan Circovic wachezaji wa timu hiyo watakaoachwa kwenye usajili msimu huu watajulikana kuanzia leo.

Kwa mujibu wa Ofisa Habari wa timu hiyo, Ezekiel Kamwaga pazia hilo la usajili litafunguliwa na kocha Milovan ambaye atapendekeza majina ya wachezaji watakaotemwa msimu huu.

Kamwaga alisema Simba ilikuwa inahitaji kukamilisha kwanza suala la mkataba mpya wa kocha Milovan aliyeiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa ligi Kuu Tanzania bara msimu huu ndipo waanze zoezi la usajili.

"Kocha wetu alikuwa na mkataba wa miezi sita ambao umemalizika hivi karibuni, leo hii (jana) mchana Kamati ya Utendaji tupo kwenye mchakato wa kumsainisha kocha Milovan mkataba mpya.

"Baada ya kusaini mkataba huo kocha atapendekeza majina ya wachezaji watakaobaki zoezi litakaloanza kesho 'leo' alisema Kamwaga na kuongeza kwamba kocha huyo atashirikiana na benchi zima la ufundi la timu hiyo.

Kimwaga alisema wapenzi na mashabiki wa timu hiyo watarajie usajili mzuri msimu huu ambao utaiwezesha timu yao kufanya vizuri ndani na nje ya nchi kama walivyofanya msimu huu.

24 MAY.Wanafunzi UDSM wadaiwa kuuza miili kukidhi mahitaji yao

KAMATI ya Bunge ya masuala ya Ukimwi imeelezwa kwamba ukosefu wa mikopo na uhaba wa mabweni ,unasababisha baadhi ya wanafunzi wa kike wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wauze miili yao na hivyo kuwa katika hatari ya kuambukizwa Ukimwi.

Hatua hiyo imekuja baada ya kamati hiyo iliyokuwa ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti, Rosweeter Kasikila kukutana na Uongozi wa Vyuo Vikuu vya Dar es Salaam na Mzumbe ili kujionea hali ya Ukimwi katika vyuo hivyo.

Waziri wa Afya na Chakula wa Serikali ya wanafunzi wa UDSM, Cosmas Nzowa aliiambia kamati hiyo jana jijini Dar es Salaam kwamba , wanafunzi wengi wanaonekana kwenye sehemu za starehe wakijiuza kwa sababu wameshindwa kuendesha maisha yao.

“Wamefika chuoni wakitokea mikoani wakakuta hakuna mikopo wala mabweni ya kulala na hawana ndugu hapa jijini, unategemea wafanye nini, sasa wengi wanajiuza ili kujikimu, ukitembelea sehemu nyingi za starehe utawakuta,” alisema Nzowa.

Alisema , mchana wanakwenda chuoni lakini usiku wanakuwa na shughuli nyingine za kujiongezea mapato.
Aliongeza kuwa hata wanafunzi wanaume wanapokosa mikopo na mabweni ya kulala vyuoni huwa katika wakati mgumu na kulazimika kuishi na wanawake waliowazidi umri huko mitaani.

“ Sasa huku hatufahamu kama wanafunzi hawa watakuwa salama katika maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwani ni jambo la kawaida kukuta kijana mdogo wa chuo kikuu akiishi na shugamami mtaani,” alisema Nzowa.

Alisema ili kurekebisha hali hiyo utaratibu wa utoaji wa mikopo hauna budi kubadilishwa ili wanafunzi kabla hawajafika chuoni wawe wanafahamu kama watapata mikopo au la.
Aliongeza kuwa ,serikali iweke kipaumbele kwa kuongeza idadi ya mabweni inayolingana na wanachuo 15,000 waliopo hivi sasa.

“ Ili kuwasaidia wenzetu ambao wamekosa maeneo ya kuishi na hawana fedha, inabidi tuishi watu wanne kwenye vyumba vidogo na hivyo kusoma katika mazingira magumu,” alisema Nzowa anayesomea Shahada ya kwanza ya Sayansi ya Jamii na Kiswahili.

Aliwaambia wabunge hao kwamba, wanafunzi hao wako katika hatari ya kupata maambukizo ya virusi vya ukimwi kutokana na mazingira magumu wanayoishi.

“Tunaiomba kamati hii itutembelee chuoni ili isikilize kilio cha wanafunzi hao,”alisema.
Mratibu wa Ukimwi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Kitila Mkumbo aliieleza kamati hiyo kwamba, maambukizo katika chuo hicho baada ya kupima mwaka 2011 ni asilimia 2.3.

Makamu Mwenyekiti wa kamati, Kasikila alitaka uongozi wa chuo hicho kuwasilisha mbele ya kamati hiyo taarifa yenye kueleza matatizo mbalimbali yanayokwamisha mapambano dhidi ya Ukimwi chuoni hapo.
“Tukipata taarifa yenye changamoto mbalimbali itawasaidia wabunge kutetea Bungeni hasa katika suala zima za upatikanaji wa fedha za shughuli za Ukimwi,” alisema Kisikila.

Akichangia, Mjumbe wa Kamati hiyo na Mbunge wa Mtambile, Masoud Abdalla Salim alisema mavazi wanayovaa wanafunzi wa UDSM yanahamasisha ngono.

“ Wanafunzi wa kike katika chuo hiki hawatofautishi mavazi ya disko na ya darasani, wanatembea nusu uchi hebu jifunzeni kwa wenzenu wa Chuo cha Biashara (CBE) wamedhibiti hilo,” alisema.Naye Mbunge wa Busega, Dk Titus Kamani alisema matatizo ya kifedha ya wanafunzi wa vyuo vikuu yanaweza kuwa kuwa kichocheo cha maambukizi ya Ukimwi.
SOURCE.www.mwananchi.co.tz

Wednesday, May 23, 2012

23 MAY.Uchaguzi huru wa urais wafanyika Misri


Raia wa Misri leo wameshiriki katika uchaguzi wa kwanza huru tangu mapinduzi ya kiraia yaliomuondoa Rais Hosni Mubarak mamlakani miezi 15 iliopita.

Wapiga kura milioni 50 walikadiriwa kushiriki katika uchaguzi huu ambao usalama unapewa kipa umbele.
Baraza kuu la jeshi nchini humo ambalo lilichukuwa utawala baada ya mapinduzi ya kiraia mwezi wa Februari mwaka jana, limeahidi kuwa uchaguzi utakuwa wa huru na haki.

Nafasi ya urais imewavutia jumla ya wanasiasa 12, wenye itakadi kali za kidini, walio na msimamo wastani na mawaziri waliotumikia utawala wa aliyekuwa Rais Hosni Mubarak.
Wagombea wanaopewa nafasi nzuri kwenye uchaguzi huo ni Ahmed Shafiq, aliyekuwa kamanda wa jeshi la angani na Amr Moussa, aliyekuwa Waziri wa mambo ya nje na kiongozi wa jumuiya ya nchi za kiarabu.

Wengine ni Mohammed Mursi, kiongozi wa vugu vugu la kiislamu, Muslim Brotherhood na Abdul Moneim Aboul Fotouh, mgombea binafsi lakini ambaye pia anegemea sera za kidini.

Uchaguzi huu utafanyika kwa siku mbili kutokana na idadi kubwa ya wapiga kura na ikiwa mshindi hatapatikana, duru ya pili ya uchaguzi itafanyika j Juni tarehe 16 na 17.

23 MAY. BROGGER MTAMBONI

23 MAY.Didier Drogba kuondoka Chelsea


Mshambulizi Didier Drogba ataihama timu ya Chelsea ya England msimu huu wa joto, baada ya kukichezea klabu kwa muda wa miaka 8.

Mchezaji huyo wa Ivory Coast, na mwenye umri wa miaka 34, alifunga bao la ushindi katika fainali ya mwaka huu ya Kombe la klabu Bingwa barani Ulaya dhidi ya Bayern.

Drogba atakuwa huru kujiunga na klabu chochote kile, kwani mkataba wake na timu ya Blues unaelekea kumalizika.

Baada ya miezi mingi ya mashabiki kutojua hatma yake, Drogba amethibitisha sasa ataondoka Stamford Bridge.

"Nilitaka kukomesha hali hii ya shaka na kuthibitisha kwamba ninaondoka Chelsea", alielezea Drogba katika tovuti ya Chelsea.

"Umekuwa ni uamuzi mgumu sana kwangu, lakini ni fahari kwangu kwa ufanisi tulioweza kupata, lakini wakati umewadia kwa changamoto mpya", alielezea.

Aliongezea: "Kama timu, tumefanikiwa katika mengi, na tukishinda vikombe muhimu."

"Ningelipenda kuitumia nafasi hii kuwashukuru wote katika klabu, hasa Roman Abramovich na wachezaji wenzangu."

Tatizo la mkataba wa Drogba ulianza msimu uliopita, wakati klabu kilipokataa kumuongezea miaka miwili zaidi katika mkataba wake.

Wasiwasi wa mashabiki ulizidi wiki chache zilizopita, iwapo Drogba ataendelea kuichezea Chelsea, hasa baada ya timu yake kuibuka mshindi katika fainali ya Kombe la FA dhidi ya Liverpool, na pia alipofunga bao la kusawazisha Jumamosi, na vilevile kufunga goli la ushindi wakati wa mikwaju ya penalti baada ya dakika 120 kumalizika kwa sare ya 1-1 dhidi ya Bayern

Tuesday, May 22, 2012

22 MAY.Matibabu ya Sajuki kitendawili


Jumapili iliyopita msanii huyo aliondoka hapa nchini kuelekea Hospitali ya Saifee iliyopo nchini India kwa matibabu, ameshindwa kufanyiwa upasuaji mapema nchini huko alikokwenda kwa dhumuni la kupata matibabu.

Kwani hali ya msanii huyo imezidi kutengemaa kila kukicha, watanzania wote kwa ujumla wameombwa kuzidi kumuombea Msanii huyo aweze kurudi haraka katika hali yake ya kawaida.

Si mwingine bali ni yule Msaniiw a Filamu za hapa nyumbani na pia ni mtayarishaji mashuhuri wa filamu hizo Salum Juma Kilowoko ‘Sajuki’, ameshindwa kufanyiwa upasuaji mapema nchini India alikokwenda kwa matibabu.

Msanii huyo anasumbuliwa na tatizo la uvimbe pembeni ya ini, ambapo wataalamu wa afya wanadai kuwa ni dalili za ugonjwa wa Hepatoma (kansa ya ini).

Hapo wawali Sajuki alianza kwa kupata uvimbe sehemu tofauti katika mkono wake mmoja, lakini baadaye tatizo hilo lilihamia ndani na kuanza kupata maumivu makali pembeni ya ini.

Kwani Msanii huyo alikaririwa akisema kwamba madaktari walibaini ana uvimbe pembeni ya ini, tatizo ambalo limekuwa likinisumbua kwa muda mrefu.

Kutokana na hali hiyo, wadau mbalimbali wa Filamu wakiwemo wasanii waliweza kumchangia nyota huyo kiasi cha fedha ambacho alitakiwa kukipata ili kuweza kufanyiwa matibabu nje ya Tanzania.

Timu nzima ya HAPA NDIO KILA KITU inazidi kumuombea msanii huyo afanyiwe mapema upasuaji huo ili arudi katika hali yake ya kawaida na kuendelea na kazi zake alizokuwa akizifanya hapo awali.