Mechi ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting ambayo ilibidi ichezwe uwanja wa taifa siku ya kesho ya Jumamosi ya tarehe 12 Agosti kwenye uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam imehamishwa ambapo sasa itachezwa kwenye dimba la Chamazi.
Maamuzi hayo ya kubadilisha uwanja kwa ajili ya mechi hiyo ya kirafiki, yametokana na kuwepo kwa shughuli ya kiserikali kama ambavyo Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa amethibitisha wakati akiongea na blog hii
“Mechi imebadilishwa tutachezea Azam Complex Chamazi lakini muda ni ule ule. Sababu ni kuwa serikali imesitisha michezo yote miwili kesho na keshokutwa kwenye uwanja wa taifa kutokana na kesho kuna shughuli ambapo viongozi wote wa serikalini watakuwepo kule upande wa pili wa uwanja kwahiyo wasingependa kuona kuna shughuli nyingine inaendelea huku (uwanja wa taifa).
“Tumeongea na uongozi wa Uwanja wa Chamazi ambapo wameturuhusu kwahiyo kesho tutachezea kule (Chamazi)”, alithibitisha Mkwasa.
Yanga na Ruvu Shooting watakutana kwenye mchezo wa kirafiki wa kujipima ngumu siku ya kesho kabla ya mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara kuondoka Jumapili asubuhi kuelekea visiwani Zanzibar ambapo watacheza mchezo mwingine dhidi ya Mlendege FC kwenye uwanja wa Amaan Jumapili Jioni kabla ya kuelekea kisiwani Pemba kwa ajili ya kambi ya kujiandaa na mchezo wa ngao ya Jamii dhidi ya Simba Agosti 23.
No comments:
Post a Comment