tuwasiliane

Tuesday, August 1, 2017

Azam FC kuweka kambi Uganda

ZIKIWA zimesalia siku 25 kabla ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kuanza, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuweka kambi ya siku 10 nchini Uganda kuanzia Jumapili ijayo Agosti 6 mwaka huu.
Kambi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya mwisho Azam FC kuelekea msimu ujao wa ligi, ambapo mabingwa hao wamepangwa kuanza kutifuana na Ndanda ya Mtwara katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona Agosti 26 mwaka huu.

Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz Ofisa Habari wa timu hiyo, Jaffar Idd, alisema kikosi hicho kikiwa nchini humo kinatarajia kucheza mechi nne kubwa za kirafiki na vigogo wa nchi hiyo, KCCA, SC Villa, Vipers na URA.
“Kama manvyofahamu kuwa mazoezi yanakwenda na mechi za kirafiki za kujaribu na kuangalia kitu umefanya, kwa hiyo tutapokuwa Uganda tunatarajia kucheza na timu za KCCA, SC Villa, Vipers na URA, kadiri siku zitakavyokwenda tutazidi kuwapa tarehe za kucheza mechi hizo,” alisema.
Alisema kikosi hicho kitakaporejea nchini Agosti 15 mwaka huu, kinatarajia kufanya maandalizi ya mwisho kabisa kabla ya ligi hiyo kuanza.
Hiyo itakuwa ni ziara ya tatu ya Azam FC ya maandalizi, ya kwanza ilikuwa ni ile ya nchini Rwanda ilipokwenda kucheza na mabingwa wa Taifa hilo, Rayon Sports na kupoteza kwa mabao 4-2, na Alhamisi iliyopita ilimaliza ziara nyingine ya Nyanda za Juu Kusini.
Katika ziara hiyo ya Nyanda za Juu Kusini, Azam FC ilicheza jumla ya mechi tatu za kirafiki, ikianza kutoka suluhu na Mbeya City, ikafungwa na Njombe Mji mabao 2-0 kabla ya kumaliza kwa kuichapa Lipuli ya Iringa mabao 4-0.

No comments:

Post a Comment