Friday, July 28, 2017
YANGA YAMPA NAFASI NYINGINE MATHEO, ASAINI MIAKA MIWILI
KLABU ya Yanga imeghairi mpango wa kumuacha mshambuliaji wake, Matheo Anthony Simon na kuamua kumrejesha kundini, ikimsainisha mkataba mpya wa miaka miwili.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika amekiambia chanzo chetu kwamba Matheo amerejeshwa kundini baada ya mwalimu, Mzambia George Lwandamia kuridhia kumpa nafasi nyingine.
Yanga ilikwishaamua kuachana na Matheo baada ya misimu miwili tangu imsajili kutoka KMKM ya Zanzibar na kushindwa kuonyesha umuhimu wake kwenye klabu.
Hata hivyo, Matheo atalazimika kutafuta jezi nyingine ya kuvaa, kwa sababu nambari 10 aliyokuwa anavaa amepewa mshambuliaji mpya, Ibrahim Hajib aliyesajiliwa kutoka kwa mahasimu, Simba.Pamoja na Matheo jana kusaini mkataba mpya wa miaka miwili na kwenda Morogoro kuungana na timu kambini, kiungo mpya Papy Kabamba Tshitshimbi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) naye ameripotiwa kusaini mkataba wa miaka miwili baada ya kufuzu vipimo vya afya.
Yanga ilivutiwa na Tshishimbi baada ya kumuona akiichezea Swallows katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Soka Afrika mapema mwaka huu Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Baada ya hapo ikamfuatilia kwenye mchezo wa marudiano Swaziland ambao aliingoza Mbabane Swallows kuichapa Azam 3-0 na kusonga mbele. Tangu hapo, Yanga imekuwa na mawasiliano na mchezaji huyo kwa lengo la kumsajili, ndoto ambazo zimetimia.
Na Nyika pia amesema wapo kwenye hatua za mwishoni kukamilisha usajili wa kiungo Raphael Daudi Loth kutoka Mbeya City ya Mbeya.
Wachezaji wengine wapya waliosajiliwa Yanga ni makipa Mcameroon Youth Rostand kutok African Lyon iliyoshuka Daraja, Ramadhan Kabwili aliyepandishwa kutoka timu B, beki Abdallah Hajji kutoka Taifa Jang’ombe na kiungo Pius Buswita kutoka Mbao FC.
Tshishimbi na Matheo wanakwenda kambini leo Morogor kufanya idadi ya wachezaji 20 waliopo huko, wengine ni makipa Youthe Rostand na Ramadhani Kabwili, mabeki Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’. Kevin Yondan, Juma Abdul, Pato Ngonyani, Andrew Vincent ‘Dante’, Mwinyi Mngwali na Abdalla Haji ‘Ninja’. Viungo ni Said Juma ‘Makapu’, Emmanuel Martin, Juma Mahadhi, Geoffrey Mwashiuya, Hussein Akilimali, Pius Buswita na washambuliaji Ibrahim Ajib na Tambwe.
Wachezaji wanne watajiunga na timu baadaye kambini Morogoro, ambao ni kipa Beno Kakolany, beki Hassan Kessy na Wazimbabwe, kiungo Thabani Kamusoko na mshambuliaji Donald Ngoma.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment