RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi anayemaliza muda wake, ameishukuru Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk. John Pombe Joseph Magufuli, wadhamini mbalimbali, washirika na wadau wa soka kwa ushirikiano walioutoa katika kipindi chote cha uongozi wake.
Taarifa ya Malinzi kupitia kwa mawakili wake, Kampuni Rwegoshora leo imesema kwamba ana imani viongozi watakaochaguliwa katika uchaguzi wa Agosti 12 mjini Dodoma watatilia mkazo mambo muhimu katika soka ya Tanzania, ikiwemo soka ya vijana na wanawake, maandalizi ya Fainali za vijana ya umri wa miaka 17 Afrika mwaka 2019 na kuboresha miundombinu ya mchezo kwa ujumla.
Malinzi amewatakia Wajumbe wa Mkutano Mkuu na wagombea wote uchaguzi mwema utakaofungua ukurasa mpya katika soka ya Tanzania. Ikumbukwe, Malinzi alilazimika kujiondoa kwenye uongozi wa TFF na kushindwa kutetea nafasi yake baada ya kuwekwa rumande tangu Juni 29 kwa tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Malinzi, Katibu wake, Selestine Mwesigwa pamoja na Mhasibu wa TFF, Nsiande Isawafo Mwanga walipelekwa rumande Juni 29 baada ya kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam.
Katika mashitaka hayo, 25 yanakwenda moja kwa moja kwa Rais wa shirikisho hilo, Malinzi akidaiwa kughushi michakato mbalimbali ya kifedha, huku matatu yakiwahusu wote na Katibu wake na Mhasibu wake Nsiande Isawafo Mwanga.
Malinzi aliingia madarakani TFF Oktoba mwaka 2013 baada ya kupata kura 72 kati ya 126 zilizopigwa akimshinda aliyekuwa mpinzani wake wa karibu, Athumani Nyamlani.
Lakini baada ya kesi hii kuanza kuunguruma na kuwekwa rumande, Kamati ya Utendaji ya TFF ilikutana na kumteua Makamu wake, Wallace Karia kukaimu Urais wa shirikisho hilo.
Karia naye yupo hatarini kuenguliwa katika uchaguzi baada ya kuitwa Idara ya Uhamiaji ya Taifa kuthibitisha uraia wake, akidaiwa kuwa ni raia wa Somalia. Mwenyewe amekiri kuwa na asili ya Somalia, lakini amekataa kuwa si Mtanzania. Uhamiaji inaendelea na uchunguzi dhidi yake.
No comments:
Post a Comment