tuwasiliane

Tuesday, January 10, 2017

AZAM KUCHEZA NUSU FAINALI LEO HUKU IKIWA NA REKODI YA HATARI,SIMBA NA YANGA HAWAJAWAHI KUIFIKIA

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kesho Jumanne saa 10.15 jioni itakuwa na kibarua kizito cha kusaka fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, itakapochuana na Taifa Jang’ombe kwenye mchezo wa nusu fainali utakaofanyika Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Azam FC inaenda kucheza hatua hiyo ikiwa imeweka bonge la rekodi kwenye michuano hiyo baada ya kuwa ndio timu pekee yenye safu ngumu ya ulinzi kutokana na kutoruhusu wavu wake kuguswa ndani ya dakika 270 (sawa na mechi tatu).
Safu ya ulinzi ya Azam FC chini ya mabeki wa kati Mghana Yakubu Mohammed na Aggrey Morris, imefanya kazi kubwa sana kwenye michuano hiyo baada ya kutengeneza uelewano mkubwa na kufanya wawe kigingi kikubwa kwa washambuliaji wa timu pinzani, ambao wameshindwa kabisa kuipenya.
Mohammed aliyesajiliwa dirisha dogo la usajili akitokea Aduana Stars ya Ghana, ameonyesha ustadi mkubwa kwenye uokoaji wa mipira ya juu akishirikiana na Morris, jambo kubwa linalombeba amekuwa akitumia akili zaidi katika kuzuia mashambulizi na pale panapohitajika nguvu amekuwa akifanya hivyo.
Langoni kipa Aishi Manula, ameanza kurejesha hali ya kujiamini hali ambayo imemfanya kuokoa michomo kadhaa hatari langoni, huku mabeki wa pembeni, Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Abdallah Kheri, nao kwa nyakati tofauti walizocheza wamefanikiwa kuonyesha uwezo mkubwa wa kuzuia mashambulizi kutokea pembeni mwa uwanja.
Katikati ya uwanja kwenye eneo la ukabaji, kiungo mpya wa nafasi hiyo, Stephan Kingue Mpondo aliyetokea Coton Sports (Cameroon), naye amekuwa mhimili mkubwa katika eneo la ukabaji huku pia akiwa ni kiungo pekee mwenye asilimia 80 za kupiga pasi zinazofika kwa mlengwa (accurate pass).
Mpondo ametengeneza kombinesheni nzuri na viungo wenzake, Frank Domayo ‘Chumvi’, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambao ndio wamekuwa watu muhimu kwa Azam FC katika kupeleka mashambulizi mbele wakishirikiana na mawinga Joseph Mahundi ‘Benteke’, Enock Atta Agyei na Sure Boy ambaye amekuwa pia akitumika kama winga wa kulia.
Kabla ya kuingia kwenye michuano hiyo, Azam FC ilitoka kucheza mechi tatu za mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) na kuruhusu bao moja tu kwenye mechi ya ugenini dhidi ya Majimaji (1-1), ilitoka suluhu na African Lyon (0-0) kabla ya kuichapa Tanzania Prisons (1-0).
Kurudia rekodi Kagame Cup
Kama Azam FC ikiendelea na mwendo huo, huenda ikarudia rekodi yake ya mwaka jana ilipotwaa ubingwa wa kwanza wa michuano ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) bila kuruhusu wavu wake kuguswa kwenye mechi sita ilizocheza hadi kuichapa Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0 katika fainali.
Itakumbukwa kuwa Azam FC pia ilitwaa taji la kwanza la Ligi Kuu msimu wa 2013/14 bila kupoteza mchezo wowote kwenye mechi 22 za ligi hiyo.
Uelekeo nusu fainali MC
Azam FC itaingia hatua hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kuifunga Yanga mabao 4-0 kwenye mchezo wake wa mwisho wa Kundi B, huku Jang’ombe nayo ikifunga pazia la Kundi A kwa kuivua ubingwa URA baada ya kuipiga bao 1-0.
Mara ya mwisho timu hizo kukutana, ilikuwa ni Julai 31 mwaka jana kwenye mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu huu, Azam FC ikishinda bao 1-0 lilifungwa na mshambuliaji aliyekuwa katika majaribio Mburundi Fuadi Ndayisenga.
Azam FC ikitinga hatua ya fainali itakayofanyika Januari 13 saa 2.15 usiku, itakutana na mshindi wa nusu fainali ya pili kati ya mechi nyingine kali ya mahasimu wa jiji la Dar es Salaam, Simba na Yanga, itakayofuatia saa 2.15 usiku.

No comments:

Post a Comment