Yanga Sc
Yanga imepaa hadi kileleni mwa msimamo wa ligi kuu Tanzania bara mara baada ya ushindi wa magoli 3-0 dhidi ya JKT Ruvu   katika mchezo wa kwanza wa raundi ya pili uliochezwa kwenye uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kwa ushindi huo, Yanga inafikisha pointi 36 baada ya kucheza mechi 16 na kuishusha Simba iliyomalizia kileleni mzunguko wa kwanza kwa pointi zake 35. Lakini Simba inaweza kurejea kileleni kesho ikishinda dhidi ya wenyeji, Ndanda FC mjini Mtwara.
Deusi Kaseke alifunga goli la kwanza la Yanga dakika ya 37 kipindi cha kwanza kwa kuunganisha pasi ya Simon Msuva .
Katika mchezo huo uliochezeshwa na Heri Sasii aliyesaidiwa na Hellen Mduma na Kassim Mpanga wote wa Dar es Salaam hadi mapumziko Yanga walikuwa mbele kwa bao 1-0.
Msuva akafunga bao la pili dakika ya 57 kabla ya kufunga tena dakika ya 90 na kuilaza JKT Ruvu huku Yanga ikikaa kileleni mwa ligi ikisubiri matokeo ya Simba.
Msuva alikuwa kwenye ubora wake kwenye mchezo dhidi ya maafande wa JKT Ruvu na hiyo inatokana na kufunga magoli mawili na kuwezesha bao moja ambalo lilifungwa na Kaseke.
Kocha George Lwandamina amepata ushindi wa kwanza katika mechi yake ya kwanza Ligi Kuu baada ya kupoteza mchezo wa kirafiki wa kujipima nguvu dhidi ya JKU ya Zanzibar uliochezwa December 10 kwenye uwanja wa Uhuru.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm alikuwepo jukwaa kuu kufuatilia mchezo, wakati kiungo mpya kutoka Zambia, Justin Zulu alikuwa jukwaani kwa sababu bado hajapatiwa kibali cha kufanya kazi nchini. 
Baada ya mchezo, kocha Lwandamina alisema timu haijaanza kucheza kwa kiwango chake kwa kuwa bao anajaribu wachezaji.
Matokeo ya mechi nyingine za Ligi Kuu leo; Mzima. Mwadui imeilaza 1-0 Toto Africans Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Mbeya City imelazimishwa sare ya 0-0 na Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Ruvu Shooting imetoka sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani.