tuwasiliane

Sunday, December 18, 2016

SIMBA YAITUNGUA NDANDA 2-0 NA KUREJEA KWENYE USIKANI WA LIGI

Nyota wa Simba wakishangilia ushindi wao dhidi ya Ndanda
Simba imerudi kileleni mwa msimamo wa ligi ya Vodacom kwa kishindo baada ya kuifunga Ndanda FC, ya Mtwara mabao 2-0, katika mchezo wa mzunguko wa 16 uliopigwa uwanja wa Nagwanda Sijaona Mtwara.
Matokeo hayo yameifanya Simba kufikisha pointi 38, na kurudi kileleni baada ya jana kuenguliwa kwa muda na mabingwa watetezi Yanga ambao waliifunga mabao 3-0 timu ya JKT Ruvu.
Wenyeji Ndanda FC, ndio waliouanza mchezo huo kwa kasi na kufanya shambulizi kali dakika ya kwanza lakini mchezaji bora wa mwezi Novemba Rifati Said alishindwa kumfunga kipa mpya Daniel Agyei aliyeudaka mpira huo kiufundi kabisa.
Wanakuchele walifanya shambulizi jingine katika dakika ya nne ya mchezo ambapo beki wa kushoto Paul Ngalema alipanda mbele kuongeza mashambulizi na alipata nafasi nzuri ya kuifungia timu yake bao la kuongoza lakini mpira alioupiga ulidakwa na kipa Agyei.
Baada ya kuokoa mashambulizi hayo Simba iliweza kufanya shambulizi la kwanza kwenye lango la Ndanda na Shizza Kichuya aliweza kupiga krosi nzuri dakika ya sita, lakini mshambuliaji raia wa Ivory Coast Fredrick Blagnon, alishindwa kuunganisha vyema kichwa chake na mpira kutoka nje.
Katika dakika ya 11, kipa wa Simba Agyei alilazimika kufanya kazi ya ziada ya kumzuia mshambuliaji wa Ndanda          Saidi aliyekuwa anakwenda kufunga baada ya kumlamba chenga yeye na mabeki wake lakini kipa huyo akaweza kudaka mpira huo miguuni kwake.
Katika dakika ya 15 mchezo ulilazimika kusimama kwa muda baada ya kiungo mpya wa Simba James kotei, kugongana na Kigi Makasi na kushindwa kuendelea na mchezo na nafasi yake kuchukuliwa na Muzamiru Yasini.
Mchezo huo uliendelea baada ya Muzamiru kuingia na katika dakika ya 23 Omary Mponda alipata nafasi nzuri lakini akashindwa kufunga baada ya shuti lake kudakwa kiufundi na kipa Agyei.
Baada ya kuingia Muzamiri Simba ilionekana kubadilika kiuchezaji na kuanza kutengeneza nafasi nyingi za mabao kwenye lango la Ndanda na dakika ya 33 Blagnon alipoteza nafasi nyingine ya wazi baada ya kichwa alichopiga kutoka nje ya lango.
Kipa wa Ndanda FC Jeremia Kisubi naye alifanya kazi ya ziada katika dakika ya 44 baada ya kupangua shuti kali la Ibrahim Ajibu na mpira kutoka nje, shambulizi hilo lilitokana na pasi nzuri ya Mohamed Ibrahim ambaye leo alionekana akifanya kazi kubwa ya kutengeneza nafasi.
Mchezo huo uliendelea kutawaliwa na wenyeji Ndanda katika kipindi cha kwanza huku Simba wakionekana kucheza kwa kujilinda ziaidi lakini hadi mapumziko matokeo yalikuwa 0-0.
Kipindi cha pili timu zote ziliuanza mchezo taratibu huku zikisomana na kufanya mashambulizi ya kustukiza ambayo hayakuwa na madhara kwa pande zote mbili.
Katika dakika ya 59, Kichuya ambaye leo alikuwa kabanwa vilivyo alishindwa kumalizia nafasi ya wazi baada ya kutengenezewa pasi nzuri na Mohamed Ibrahim.
Mambo yalianaza kuwabadilikia wenyeji Ndanda baada ya Mzamiru Yasini kuifungia Simba bao la kuongoza dakika ya 63, baada ya kupokea pasi nzuri ya Mohamed Ibrahi na kuachia shuti kali lililomshinda kipa Kisubi wa Ndanda.
Bao hilo lilionekana kuwaongezea kasi Simba na kuendelea kupambana kutafuta bao jingine lakini Ndanda walikuwa makini kuondosha hatarizote langoni mwao.
Kocha Selemani Matola alimtoa mshambuliaji wake Omory Mponda na kumuingiza Salum Mineli ili kwenda kuongeza kasi ya mashambulizi kwenye lango la Simba lakini mambo hayakuwa rahisi kama Matola alivyotarajia.
Mabadiliko hayo yalionekana kuimuza Ndanda kwani dakika ya 81 Mohamed Ibrahim alifunga bao la pili kwa Simba na kupoteza matumaini ya wenyeji waliokuwa wamepania kupata angalau sare kwenye mchezo huo.
Ndanda waliendelea kupambana kutafuta angalau bao moja lakini hadi dakika 90 za mchezo huo zinakamilika Simba waliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

No comments:

Post a Comment