Joseph Omog - Simba
Kiungo mpya wa klabu ya Simba James Kotei , anaweza kurudi Uwanjani Disemba 24, kuwakabili JKT Ruvu , baada ya kushindwa kumaliza dakika zote 90, katika mchezo wake wa kwanza kutokana na kuumia.
Daktari wa Simba, Yassin Gembe amekiambia chanzo kimoja kuwa , mchezaji huyo anaendelea vizuri na kunauwezekano kubwa Jumamosi mchezaji huyo akacheza dhidi ya JKT Ruvu.
“Kotei anaendelea vizuri na ameshaanza mazoezi na wenzake na tunaendelea kuifatilia afya yake kwa karibu ninaimani hadi kufika siku ya mchezo atakuwa ameimarika zaidi,”amesema Gembe.
Mchezaji huyo alicheza kwa dakika 13, kabla ya kugongana na nahodha wa Ndanda FC, Kiggi Makasi na kushindwa kuendelea na mchezo na nafasi yake kuchukuliwa na Muzamiru Yasini.

Kocha wa Simba Joseph Omog, amefuraishwa na uchezaji wa mchezaji huyo na angependa kumpa nafasi nyingine ya kuanza kwenye mchezo ujao
Omog amesema Kotei, alicheza vizuri na kusaidia vyema safu ya ulinzi kama anavyotaka ndiyo maana ya kuhimiza mchezaji huyo kupona mapema ili aweze kumpanga kwenye mchezo wao wa Jumamosi.
“Unajua nimchezaji mpya ndiyo kwanza ameingia kwenye timu ndiyo maana tunataka kumpa nafasi mara kwa mara ili ili aweze kuzoeana na wenzake pamoja na falasafa ya timu na ameonyesha uwezo mkubwa kwenye dakika 13 alizocheza dhidi ya Ndanda FC, kabla hajaumia,” amesema Omog.
Mchezaji huyo anakabiliwa na ushindani mkubwa kutoka kwa Jonas Mkude ambaye ndiyo nahodha wa timu hiyo anayeimudu vyema nafasi hiyo kwa muda mrefu tangu apandishwe timu ya wakubwa akitokea Simba B.
Kotei ametua Simba akitokea nchini Oman,alipokuwa akicheza soka la kulipwa kwenye moja ya klabu nchini humo lakini mambo yalimwia magumu na kuamua kutafuta timu nyingine na kufanikiwa kutua Simba.