tuwasiliane

Wednesday, December 14, 2016

NDOA' YA AZAM, MIGI YAFIKA TAMATI, SOMA ALICHOSEMA MENEJA


KIUNGO wa Azam FC, Jean Baptiste Mugiraneza 'Migi' yuko mbioni kutimka klabuni hapo baada ya uongozi wa klabu hiyo kugoma kumuongezea mkataba wa miaka miwili na sasa mkataba wake utavunjwa muda wowote kuanzia sasa.

Migi alijiunga na Azam, Julai mwaka jana akitokea APR ya Rwanda ambapo mkataba wake utafikia tamati mwishoni mwa msimu huu ambapo kocha wa timu hiyo Mhispania Zeben Hernandez ameagiza kutoongezewa mkataba mchezaji yoyote mpaka mwisho wa ligi ili awafanyie tathimini kabla ya kuingia mikataba mipya.


Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba alisema mkataba wa mchezaji huyo umebaki miezi sita na tayari suala lake limepelekwa kwa viongozi ili lijadiliwe.


"Kuhusu suala la mchezaji kutaka kuondoka sisi tunasikiliza taarifa ya kocha kwahiyo Migi bado ni mchezaji wetu suala lake limeletwa tunalifanyia kazi mwisho wa siku kila kitu kitakaa sawa," alisema Kawemba.


Endapo Migi ataachana na Azam ataungana na nyota kadhaa wa kimataifa walioondoka klabuni hapo ambao ni Kipre Tchetche, Michael Balou, Didier Kavumbagu, Alan Wanga na Pascal Wawa. Na tayari wamewapa mikataba wachezaji wawili wa kigeni ambao ni Enock Atta Agyei na Yahaya Mohamed. 


Wakala wa mchezaji huyo, Claver Kazungu aliiambia BOIPLUS kuwa ''Ni kweli tunavunja mkataba na Azam na sasa tunasubiri wamlipe haki zake zote za kimkataba ikiwemo mishahara ya miezi iliyobaki kwenye mkataba wake.


"Migi ni mchezaji wa hali ya juu, ni mzoefu na amecheza timu ya Taifa kwa miaka 11 hivyo hawezi kukosa timu ya kucheza, timu zipo nyingi na atapata tu," alisema Kazungu.


Azam wamemaliza duru la kwanza wakiwa katika nafasi ya tatu baada ya kujikusanyia pointi 25 ambapo Jumapili ijayo watakuwa wageni wa African Lyon kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam katika mechi yao ya kwanza ya mzunguko wa pili wa ligi.

No comments:

Post a Comment