tuwasiliane

Friday, December 2, 2016

Juma Kaseja asaini Kagera Sugar

kipa wa Mbeya City, Juma Kaseja aidaka
Kipa mkongwe aliyewahi kuzidakia klabu za Simba na Yanga Juma Kaseja, ametua timu ya Kagera Sugar kwa mkataba wa mwaka mmoja baada ya kuwa huru tangu alipomaliza mkataba wake na Mbeya City mwishoni mwa msimu uliopita.
Mratibu wa Kagera Sugar Mohamed Hussein, amekiambia chanzo chetu kuwa, wameamua kumsajili kipa huyo wakiamini ni kipa mzuri mwenye uwezo wa kuirudisha timu yao kwenye ubora wake iliyokuwa nayo siku za nyuma.
“Nikweli tumemsajili Kaseje, kwa mkataba wa mwaka mmoja na tayari yupo kambini tupo naye kambini tukijiandaa na mzunguko wa pili wa ligi ya Vodacom ambao umepangwa kuanza Desemba 17,”amesema Hussein.
Kiongozi huyo amesema usajili wa Kaseja umebarikiwa na kocha wao mkuu Mecky Maxime ambaye hivi karibuni katika ripoti yake ya kumalizika kwa mzunguko wa kwanza alipendekeza timu hiyo kusajili kipa mmoja mwenye uzoefu ili kusaidiana na waliopo.Amesema baada ya kutua kwa Kaseja, sasa wamepanga kumuachia kipa wao Hussein Shariff, ‘Cassilas’ ambaye walimsimamisha kwa muda usiojulikana kutokana na tuhuma za kuuza mechi na kusababisha kufungwa mabao 6-2 na mabingwa watetezi Yanga kwenye uwanja wa Kaitaba Kagera.
“Bado hatujatangaza rasmi lakini tunafikiria kumruhusu aende ambapo anaweza kupata timu ya kucheza kwasababu tayari tumepata mbadala wake na tunaimani na Kaseja kwasababu ni kipa mwenye uzoefu na anaijua vizuri ligi ya Vodacom naamini atatusaidia kutufikisha kule tunapopataka,”amesema Hussein.
Kaseja alikuwa mchezaji huru na mara ya mwisho alikuwa kipa wa timu ya taifa ya mchezo wa soka beach, ambayo ilitolewa na Ivory Coast kwenye michuano hiyo iliyofanyika katikati ya mwaka huu na baada ya hapo mchezaji huyo alipata nafasi ya kuwa kocha wa makipa wa timu ya taifa ya Vijana ‘Serengeti Boys’ iliyoshindwa kufuzu fainali za AFCN zitakazo fanyika 2017 Madagascar.

No comments:

Post a Comment