tuwasiliane

Sunday, December 25, 2016

AZAM;‘Tutafika mbali zaidi CAF’


BAADA ya kuiona ratiba ya Kombe la Shirikisho Afrika mwakani iliyotoka juzi jioni, Kocha Mkuu wa Azam FC, Zeben Hernandez, ameweka wazi kuwa amekipanga kikozi chake kufika mbali zaidi kwenye michuano hiyo.
Kwa mujibu wa droo hiyo, Azam FC kwa mara ya pili mfululizo imepangwa kuanzia raundi ya kwanza ya michuano hiyo, ambapo itakutana na mshindi wa jumla wa mechi ya raundi ya awali kati ya Orapa United ya Botswana na Mbabane Swallows ya Swaziland.
Azam FC iliyojiwekea malengo ya kuingia hatua ya makundi ya michuano hiyo, itaanza kucheza ugenini na moja timu hizo kati ya Machi 10 hadi 12 mwakani kabla ya kurejeana nyumbani Azam Complex kati ya Machi 17 na 19.
Mabingwa hao wa Ngao ya Jamii wakifuzu hapo, wataingia raundi ya mwisho ya mtoano (play off), watakayocheza na moja ya timu 16 zilizotolewa kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikivuka mtihani itaingia moja kwa moja kwenye hatua ya makundi.
Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz Hernandez, alisema kuwa kutokana na usajili uliofanywa na namna kikosi chake kinavyoimarika anauhakika watafika nafasi ya juu zaidi tofauti na malengo iliyojiwekea timu hiyo.
“Tumefurahi namna ratiba ilivyopangwa, tumeanzia raundi ya kwanza kutokana na ubora wa Azam FC tofauti na timu nyingine zilizoanzia raundi ya awali, kiufupi malengo makubwa tumepanga kufika juu zaidi ya hatua ya makundi, namna gani tutafikia ni kutokana na wachezaji waliosajiliwa hivi sasa kuwa na uzoefu mkubwa na ni wachezaji wazuri na tunaamini wanaweza kutufikisha huko tunapokusudia,” alisema.
Kocha huyo alisema kuwa ili kufikia huko, lazima kazi kubwa ifanyike na kila mtu kuweza kujituma kwenye nafasi yake huku akidai kuwa kwa sasa watajitahidi kujipanga vilivyo kwa ajili ya mechi za michuano hiyo ikiwemo kuwafanyia tathimini wapinzani wao ambao mmojawapo wanatarajia kucheza naye.
“Naamini ya kuwa kwa sasa ni muda mzuri wa kujipanga zaidi, haya ni mashindano mazuri na makubwa kinachotakiwa ni sisi kuingia tukiwa tayari tumeshajipanga vizuri, ili ushiriki wetu uweze kuwa mzuri na hatimaye kufika nafasi za juu zaidi,” alisema.

No comments:

Post a Comment