tuwasiliane

Friday, December 30, 2016

Azam FC yafanya ziara Aga Khan Hospital

KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo imefanya ziara ndefu kwenye moja ya Hospitali bora nchini ya Aga Khan iliyopo jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo ilikuwa ni maalumu kwa ajili ya wachezaji na benchi la ufundi la timu hiyo kujifunza namna hospitali hiyo inavyotoa huduma za kila siku kwenye vitengo vyake mbalimbali vikiwemo vya wagongwa wa figo, saratani, mifupa.
Mbali na kujionea hayo, pia walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali ya kiafya juu ya kazi yao ya soka na wataalamu wa hospitali hiyo waliweza kuwajibu kitaalamu na kuwapa ushauri wa namna ya kutunza miili yao ili waweze kudumu katika soka.
Baada ya kujifunza mambo mbalimbali juu ya afya zao, zoezi litakalofuata kwa siku za usoni mara baada ya michuano ya Kombe la Mapinduzi, ni wachezaji wa kikosi hicho kurejea Aga Khan Hospital kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya mwili mzima.
Uongozi wa Azam FC unaendelea na mazungumzo na uongozi wa hospitali hiyo kwa ajili ya kuingia ubia wa ushirikiano, utakaowawezesha wachezaji wa timu hiyo kupata matibabu mbalimbali na kupunguza gharama za kuwapeleka Afrika Kusini kwa ajili ya kutibiwa.
Aga Khan ni moja ya hospitali za kisasa nchini zinazotoa huduma bora za tiba mbalimbali, jambo ambalo limeiwezesha kutwaa tuzo za juu za kimataifa (gold) ikiwa kama ni hospitali namba moja nchini.
Aga Khan wanasemaje?
Akizungumza wakati wa kuiaga timu hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa hospitali hiyo, Dr. Mustaafa Bapumai, aliushukuru uongozi wa Azam FC kwa kufanikisha timu hiyo kutembelea Aga Khan huku akitoa changamoto kwa wachezaji kujua afya zao kabla ya kucheza uwanjani.
“Tunawashukuru kwa kuja tena hapa, miaka ya nyuma kila mlipokuja tuliweza kujiandaa kuwafanyia matibabu, hivi sasa uongozi utakapokuwa tayari tutawapima ili kila mchezaji ajue afya yake.
“Kwa madogo haya nawashukuru sana na nawakaribisha viongozi wenu wawe huru kuja hapa kuzungumza na sisi pale wanapotaka kujua afya za wachezaji wao kwa kuwaleta wapimwe,” alisema Dr. Bapumai.
Himid Mao alonga
Nahodha Msaidizi wa Azam FC, Himid Mao, naye alitoa neno kwa upande wa wachezaji wenzake, ambapo aliushukuru uongozi wa Aga Khan kwa kuwapa elimu tosha juu ya afya zao.
“Kwanza ningependa kuchukua nafasi hii kuishukuru timu yetu na uongozi mzima wa Aga Khan Hospital, tumejifunza vitu vingi sana na vingine tulikuwa hatuvifahamu na pia tumepata mwangaza, mmetuonyesha vifaa vyenu mnavyotumia, hivyo tunawashukuru sana na tumefurahi kuwa nanyi, asanteni sana,” alisema.
Bosi Azam FC apigilia msumari
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa Azam FC, Ofisa Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Saad Kawemba, alisema kuwa watahakikisha wanakamilisha kila kitu ili kuwawezesha wachezaji wao kupatiwa matibabu ndani ya hospitali hiyo ikiwemo kujua afya zao.
“Tutashirikiana na uongozi kuhakikisha tunakamilisha hili na malengo yetu ni kuwa Aga Khan iwe ni hospitali tutakayoitumia, yaani pale tunapopata matatizo mchezaji aende Aga Khan akapatiwe matibabu na kujua afya yake, hilo ndio lengo letu kuu na tunaamini tutafanikiwa, tunapenda kuwashukuru sana,” alisema.
Suala la afya za wachezaji limekuwa likishindwa kupewa kipaumbele na timu nyingi za Tanzania, jambo ambalo limekuwa likisababisha matatizo kwa wachezaji uwanjani, mfano ni tukio la hivi karibuni la kufariki uwanjani kwa mchezaji wa timu ya vijana ya Mbao, Ismail Khalfan.
Mchezaji huyo alidondoka uwanjani baada ya kupata shambulizi ya moyo ‘Heart Attack’, wakati wa mchezo dhidi ya Mwadui kwenye kituo cha Kundi B mkoani Kagera katika michuano ya Ligi ya Taifa ya Vijana ya TFF iliyomalizika mwanzoni mwa mwezi huu.

No comments:

Post a Comment