Ajibu na Haras El Haduud
Klabu ya Simba inatarajia kutunisha mfuko wake kwa kupokea kiasi kikubwa cha fedha, ambazo itamuuza mshambuliaji wake Ibrahim Ajibu, aliyefuzu majaribio kwenye klabu ya  inayoshiriki ligi kuu nchini Misri.
Ajibu amekiambia chanzo chetu, kwa njia ya mtandao wa kijamii Facebook, akiwa Alexandria kuwa uongozi wa timu hiyo umemtaarifu kuwa amefuzu na kinachotakiwa kwa sasa ni klabu ya Simba kuzungumza kuhusu bei ambayo watamuuza kwenye timu hiyo.
"Nimefanya mazoezi kwa siku tano na jana jamaa wamenifata na kuniambia nimefaulu majaribio yao na kinachotakiwa ni uongozi wa timu yangu inayonimiliki kuongea nao ili waweze kupangiana bei ya kulipa ili waweze kunichukua na kunitumia kwenye ligi yao,”amesema Ajibu.
Mshambuliaji huyo amesema atafurahi kama uongozi wake utakamilisha mazungumzo kwa kutaja kiasi ambacho timu hiyo itaweza kukimudu na kulipa ili aweze kuondoka kwani kwa muda mrefu amekuwa akitamani kucheza soka nje ya Tanzania kama ilivyo kwa wachezaji wengi.
Mshambuliaji huyo ambaye siku za karibuni ameonekana kutokuwa na maelewano mazuri na uongozi wa timu yake ya Simba amesema angependa kubadilisha mazingira na kucheza kwake Misri siyo tu kutamsaidia yeye bali hata timu ya taifa ‘Taifa Stars’.
Amesema anaamini uongozi wake hautaweka kipingamizi katika hili na badala yake utamruhusu kama ulivyofanya wakati anakwenda kufanya majaribio nchini misri.
Simba wanalazimika kumuuza Misri mchezaji huyo kwani siku za karibuni amekuwa kuwa akihusishwa kujiunga na Yanga, jambo hilo linaweza kutokea kweli kwani amebakiza miezi minne ili kumaliza mkataba wake wa kuichezea timu hiyo hivyo kama watambania anaweza kuondoka bure akajiunga na mahasimu wao Yanga ambao wanamuhitaji kwa udi na uvumba.