tuwasiliane

Saturday, November 5, 2016

MORALI YAZIDI KUPANDA AZAM FC KUELEKEA MECHI NA MBAO FC

KOCHA Mkuu wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Zeben Hernandez, ameweka wazi kuwa morali inazidi kupanda kwenye kikosi chake kuelekea mchezo ujao dhidi ya Mbao, utakaofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, jijini hapa Mwanza kesho Jumapili.
Hali hiyo imempa matumaini makubwa Hernandez, ya kikosi chake kuibuka na ushindi katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).
“Tunaendelea kujiandaa kwa mchezo unaokuja, ukiangalia kadiri kila siku zinavyokwenda wachezaji ndio morali inaongezeka, kwa sababu lengo kubwa ni kuhakikisha tunakamilisha pointi ambazo tumekuja kuzifuata.
“Kama tulivyopata pointi katika mechi mbili zilizopita, ndivyo tunategemea kufanya katika mchezo ujao ili tuweze kukamilisha pointi katika kanda hii kabla ya kuelekea kwenye mchezo mwisho dhidi ya Mwadui (Novemba 9),” alisema Hernandez wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz
Katika hatua nyingine alizungumzia uwezekano wa kuwepo kikosini kwa nyota wake, Bruce Kangwa, aliyekuwa majeruhi baada ya kuanza mazoezi na wenzake leo, ambapo amedai kuwa uamuzi wa kurejea uwanjani katika mchezo huo ataufanya katika mazoezi ya mwisho kesho Jumamosi.
“Bruce kaonekana amefanya mazoezi na wenzake leo, kwa hiyo uhakika kama ataweza kucheza mchezo huo itakuja pale ambapo tutamaliza mazoezi ya mwisho ambayo ni kesho, baada ya hapo tutajua ufiti wake wa mwili uko vizuri kuweza kucheza mchezo unaokuja au kuna taarifa nyingine tofauti,” alimalizia.
Azam FC inayodhaminiwa na kinywaji safi kinachoburudisha koo na kuchangamsha mwili cha Azam Cola na Benki bora nchini kwa usalama wa fedha zako ya NMB, itaingia kwenye mchezo huo ikiwa imejikusanyia jumla ya pointi 22 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikizidiwa pointi 13 na kinara Simba aliyejikusanyia 35.

No comments:

Post a Comment