tuwasiliane

Sunday, November 6, 2016

Koeman akiri Chelsea imeifunza adabu Everton

Koeman akiri Chelsea imeifunza adabu Everton
Kocha wa Everton amekiri kuwa kikosi chake kilizidiwa kila kitu, kuanzia nguvu, ufundi na kasi ndio maana waliangukia pua kwa Chelsea
Ronald Koeman amekiri kuwa Everton walifundishwa somo la kucheza mpira waliponyukwa 5-0 na Chelsea Darajani Jumamosi.
Toffees walikuwa wamezidiwa kipindi chote cha mechi hiyo na hatimaye wakaambulia kipigo cha mabao mengi cha kudhalilisha kutoka kwa Blues.
“Ni somo kubwa kwa kila mmoja leo,” alisema Koeman. “Chelsea walituonyesha kwamba wana kiwango kikubwa cha soka katika kila Nyanja.
“Namna wanavyocheza kwa nguvu, ubora wanapokuwa na mpira, kupokonya mipira, kulikuwa na tofauti kubwa. Sikutarajia tofauti ile dimbani lakini imetokea.
 “Ni vema kwa kila mmoja kuona; ubora, wachezaji wenye ufundi, namna wanavyofanya kazi, kukimbia na kushambulia. Tunaweza kujifunza kutoka hapo na, hatimaye, ni kazi yangu kubadili timu au wachezaji kama nikiona kuna ulazima wa kufanya hivyo.”
Wakati Everton walionekana kucheza kwenye kiwango cha chini, wenyeji walikuwa katika kiwango cha juu, Eden Hazard akicheza katika ustadi wa hali ya juu na kufunga mabao mawili.
Na Koeman alisema alivutiwa na Chelsea, ambao wameshinda mechi tano za ligi mfululizo bila ya kuruhusu goli tangu walipanza kucheza kwa kutumia mabeki watatu.
“Wanafunga sana, hawaruhusu magoli, jambo ambalo ni sababu kubwa kwao kufanya vizuri,” alisema. “Wachezaji kadhaa muhimu katika timu yao wanaonyesha weledi wao wa hali ya juu katika soka.
 “Sijawahi kuona timu imara kama hii ikicheza tofauti na mfumo wao, ni mfumo mgumu sana unapocheza dhidi yao, mwendo wa Hazard, [Diego] Costa, Pedro… meneja ameleta akili za ushindi kwa wachezaji hawa.
“Wanaonekana wenye njaa sana katika kila mechi na kama wakiendelea hivi watapambana hadi kutwaa taji.”
Alipoulizwa ni namna gani timu yake itaamka kutokana na kipigo hicho baada ya likizo ya kimataifa, Koeman aliongeza: “Kila mmoja amevunjika moyo, lakini ni pointi tatu tu. Lakini kwa kweli tunahitaji kuamka na kujibu mapigo na kuonyesha kwamba kiwango duni cha leo si kiwango chetu, tunaweza kufanya vizuri.”

No comments:

Post a Comment