BENCHI la Ufundi la Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, limesema kuwa si kazi rahisi kwao hivi sasa kubadilisha mfumo wa 3-5-2 wanaoutumia katika mechi za mashindano mbalimbali walizocheza mpaka sasa.
Mfumo huo umekuwa ni kipenzi cha Kocha Mkuu Stewart Hall tokea akabidhiwe kibarua hicho Juni mwaka jana, ambao umemwezesha kutwaa ubingwa wa Kombe la Kagame Agosti mwaka jana pamoja na taji la michuano maalumu waliyoshiriki nchini Zambia hivi karibuni.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo dhidi ya Mwadui, Kocha Msaidizi wa Azam FC, Dennis Kitambi, alisema kuwa tatizo la timu hiyo sio mfumo kama inavyodhaniwa na wengi, huku akidai kuwa ni baadhi ya vitu vidogo tu wanavyotakiwa kubadilisha kama kutumia vema nafasi wanazozitengeneza.
“Si jambo jepesi kubadilisha mfumo hivi sasa na kuanza kutumia mwingine, ikumbukwe ya kuwa mfumo huu tumeanza kuufanyia kazi tokea mwezi Juni mwaka jana.
“Kama nilivyosema kuna baadhi ya vitu ndio vinatakiwa kufanyiwa kazi, kama ulivyoona leo tumetengeneza nafasi nyingi takribani sita hadi saba za kufunga kipindi cha kwanza dhidi ya Mwadui, lakini tumeshindwa kuzitumia,” alisema.
Matajiri hao wa viunga vya Azam Complex wanatarajia kushuka tena dimbani Jumapili hii (Februari 14) kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga kwa kuvaana na wenyeji wao Coastal Union.
Azam FC inayodhaminiwa na Benki ya NMB kwa sasa ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo wowote kwenye mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) ikiwa imecheza mechi 16, ikishinda 13 na sare tatu, ikijikusanyia jumla ya pointi 42 sawa na Simba iliyo katika nafasi ya pili.
Lakini ina mechi mbili mkononi dhidi ya wekundu hao pamoja na Yanga, ambayo ipo kileleni kwenye msimamo ikiwa imejisanyia jumla ya pointi 43, hivyo kama Azam FC itashinda viporo vyake na mechi nyingine zinawakabili katika ligi itapanda kileleni na kuongoza ligi.
No comments:
Post a Comment