tuwasiliane

Friday, January 22, 2016

Wawa: Mimi Tanzania ni Azam FC tu

BEKI kisiki wa Azam FC, Pascal Wawa, ameweka wazi kuwa hakuna timu nyingine atakayoichezea Tanzania zaidi ya klabu hiyo Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, anayokipiga kwa sasa.
Akifanya mahojiano maalumu na mtandao wa www.azamfc.co.tz hivi karibuni, beki huyo raia wa Ivory Coast alisema kuwa Azam FC ndio timu bora hapa nchini kutokana na namna inavyoendeshwa.
Wawa amesema kuwa yupo tayari kuichezea timu hiyo kwa miaka mitano ijayo, lakini si kujiunga na timu nyingine yoyote ya hapa.
“Nikipata ofa kubwa nje ya hapa Tanzania nipo tayari kuondoka, lakini si kuchezea timu nyingine ya hapa nje ya Azam FC ninayoichezea hivi sasa, hapa nilipo kuna kila kitu ambavyo havipo kwa timu nyingine, hivyo siwezi kujiunga na timu nyingine ya hapa,” alisema.
Nyota huyo aliyejiunga na kikosi hicho Desemba mwaka juzi akitokea El Merreikh, amesema kuwa malengo waliyokuwa nayo Azam FC yanaendana kabisa na timu yake hiyo ya awali kutoka Sudan, kwani wote wanazungumza lugha moja ya kufikia mafanikio.
“Azam FC ni mahali pazuri ni mwaka mmoja sasa nipo hapa, wachezaji wote walinipokea vema na kuna umoja mkubwa wa wachezaji hapa, viongozi na hata makocha, nafarahi kucheza Tanzania,” alisema.
Wawa pia alizungumzia utofauti wa soka la Tanzania na Sudan, alikokuwa akicheza awali akisema kuwa limepishana kidogo akidai Sudan kuna ushindani mkubwa, lakini jambo kubwa linawaathiri ni vita vilivyomo ndani ya Taifa hilo.
“Kuna muda mnaweza kuwa kwenye mazoezi au mechi mkasikia ndege za kivita zinapita au mabomu, ile inakuwa si hali nzuri kabisa, lakini hapa Tanzania kuna Amani kubwa na umoja pia,” alisema.
Beki huyo kipenzi wa mashabiki wa Azam FC na wapenzi wengine wa soka nchini, ndiye mchezaji pekee wa matajiri hao aliyecheza mechi zote 15 za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), ambazo imecheza mpaka sasa huku timu hiyo ikiwa nafasi ya pili kwa pointi 39 sawa na Yanga inayoongoza kileleni.

No comments:

Post a Comment