tuwasiliane

Wednesday, January 20, 2016

KIVUMBI LIGI KUU YA VODACOM LEO NA KESHO

Azam Simba Ligi Kuu Bara
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo Jumatano na kesho Alhamisi, mvuto zaidi ukiwa mechi za miamba watatu wanaofukuzana kileleni, Azam FC, Simba na Yanga SC
Yanga SC inaongoza Ligi Kuu kwa wastani wa mabao, ikiwa inalingana kwa pointi (36) na Azam FC iliyo nafasi ya pili, wakati Simba SC inafuatia ikiwa na pointi 30.
Azam FC baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na vibonde African Sports Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam wanasafiri hadi Tanga kuwafuata Mgambo JKT.
Mchezo huo unaotarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua utapigwa leo katika uwanja wa Mkwakwani na Azam FC watahitaji ushindi ili kuendelea ‘kula sahani moja’ na Yanga SC katika mbio za ubingwa.
Hali kadhalika Simba SC nao watakuwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo siku ya Jumatano kumenyana na JKT Ruvu katika mchezo ambao utawakutanisha makocha wa zamani wa Kagera Sugar, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibaden’ na Mganda Jackson Mayanja.
Kibaden, kocha na mchezaji wa zamani wa Simba SC kwa sasa anaiongoza JKT Ruvu iliyofungwa 5-1 na Mgambo JKT, wakati Mayanja atakuwa kwenye mchezo wa pili tangu arithi mikoba ya Muingereza, Dylan Kerr Simba SC.
Simba SC inaweza kumkosa mshambuliaji wake tegemeo, Ibrahim Ajib aliyeumia Jumamosi .timu hiyo ikishinda 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi nyingine za Ligi Kuu ya siku ya leo ni kati ya Stand United na Toto Africans Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Ndanda FC na Mbeya City Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara na Prisons dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Mabingwa watetezi, Yanga SC wao watashuka dimbani, kesho siku Alhamisi kumenyana na Majimaji ya Songea, iliyo chini ya kocha mpya, Muingereza mwenye asili ya Tanzania, Kalimangonga Sam Daniel Ongala.
Kali Ongala, mshambuliaji wa zamani wa Yanga SC na kocha Msaidizi wa zamani wa Azam FC, huo utakuwa mchezo wake wa pili tangu apewe timu hiyo, baada ya mwishoni mwa wiki kupata sare ya ugenini ya 1-1 na Coastal Union, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Na Yanga SC ambayo haikucheza soka la kuvutia ikishinda 1-0 dhidi ya Ndanda mwishoni mwa juma, itakutana na majaribu ya wachezaji wake wa zamani kesho, beki Lulanga Mapunda na mshambuliaji Danny Mrwanda ambao wapo Majimaji kwa sasa.
Mechi nyingine za Ligi Kuu ZA LEo ni kati ya Mwadui FC na Kagera Sugar Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga na African Sports wataikaribisha Mtibwa Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.

No comments:

Post a Comment