tuwasiliane

Sunday, January 24, 2016

Aggrey Morris sasa mambo safi, kurejea dimbani Februari 5

BEKI kisiki wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, Aggrey Morris, anayesumbuliwa na majeraha ya goti, sasa habari njema ni kwamba anatarajia kurejea dimbani Februari 5, mwaka huu.
Majeraha hayo aliyapata wakati akiwa kwenye majukumu ya timu yake ya Taifa ya Zanzibar Heroes Novemba mwaka jana, wakati ikijiandaa na michuano ya Kombe la Chalenji, iliyofanyika nchini Ethiopia.
Mwanzoni mwa wiki iliyopita beki huyo alikwenda jijini Cape Town nchini Afrika Kusini kufanyiwa uchunguzi wa majeraha hayo katika Hospitali Afrisurb na alirejea salama Jumapili iliyopita.

Akizungumza na mtandao wa klabu hiyo Daktari wa timu ya Azam FC, Juma Mwimbe, alisema kuwa beki huyo anaendelea vema na habari njema iliyopo ni kuwa amefanikiwa kukwepa upasuaji kutokana na vipimo alivyofanyiwa kule kuonyesha ya kuwa mguu wake una maumivu ya kawaida na hauhitaji upasuaji.
“Tunamshukuru Mungu mambo yameenda vizuri, kule wametuambia anaweza kuendelea na matibabu hapa nchini katika kumponya majeraha hayo, baada ya kumfanyia vipimo walibaini ya kuwa tatizo lake si kubwa na kuamua kumchoma sindano ya kuondoa uvimbe kwenye goti lake na atachomwa nyingine akiwa hapa nchini wakati anaendelea na programu ya matibabu yake,” alisema.
Mwimbe alisema kwa mujibu wa matibabu aliyofanyiwa, wataalamu wa kule wametueleza kuwa anaweza kuanza mazoezi baada ya wiki mbili zijazo (Februari 5).
“Aggrey ataanza moja kwa moja na mazoezi ya viungo gym ili kujiweka fiti kwa muda wa wiki mojakabla ya kujumuika na wenzake kama maendeleo yake yatakuwa mazuri, lakini tunaamini ya kuwa atarejea ndani ya muda uliopangwa kwani hata mchezaji mwenyewe amekuwa na hamu kubwa ya kutaka kurejea dimbani,” alisema.
Kabla ya kuelekea nchini Afrika Kusini, taarifa za awali zilizokuwa zimetoka kuhusu majeraha waliyokuwa nayo beki huyo ni kuwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji, ambao ulitarajia kumweka nje ya dimba kwa takribani miezi mitatu.

No comments:

Post a Comment