Simba Vs Azam, Yanga, Mgambo
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaendelea leo Jumamosi baada ya mapumziko ya takribani mwezi mmoja kupisha michuano ya kimataifa.
Nyasi za viwanja sita zitawaka moto siku ya leo, lakini macho na masikio ya wengi vitaelekezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambako vigogo Simba SC watakuwa wanamenyana na Azam FC.
Azam FC wanahitaji ushindi katika mchezo wa leo kujiimarisha kileleni na kuzidi kuwaacha mabingwa watetezi, Yanga SC wakati Simba SC inahitaji ushindi ili kurudi kwenye mbio za ubingwa.
Na hapo ndipo ulipolalia utamu na msisimko wa mchezo huo, kiasi kwamba hata mashabiki wa Yanga ingawa timu yao itakuwa Uwanja wa Mkwakwani  ikimenyana na Mgambo JKT, lakini watakuwa wanasikilizia kinachoendelea Taifa.
Hali kadhalika Yanga SC wanaitakia sana ushindi Simba SC au hata sare, ili mahasimu wao hao, Azam FC katika mbio za ubingwa wapunguzwe kasi.
Simba SC imeimarisha kikosi chake katika dirisha dogo kwa kumrejesha mshambuliaji wake Mkenya, Paul Kiongera aliyekuwa anacheza kwa mkopo KCB.
Akizungumza na chanzo kimoja, Kocha Mkuu wa Simba, Dylan Kerr amesema ana matarajio makubwa ya kuibuka na ushindi dhidi ya Azam FC leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Alisema anajua ugumu uliopo kwenye mchezo huo kutokana na uzuri wa wapinzani wao wenye wachezaji wengi wazoefu, lakini hilo haliwezi kuwa kikwazo cha kushindwa kupata ushindi.
“Ni mchezo mgumu, lakini wenye kuvuta hisia nyingi za mashabiki kwa sababu zinakutana timu mbili kubwa zenye ubora unaokaribiana. “Nina matumaini makubwa ya kupata ushindi, ingawa hatupewi nafasi sana kutokana na ubora wa wapinzani wetu unavyoonekana,” alisema Kerr.
Hata hivyo alisema ana uhakika wa ushindi kwenye mchezo huo na hatishwi na ukubwa wa maumbo na majina ya wachezaji wa Azam. “Tulimaliza mzunguko wa tisa kwa heshima kubwa ya kushinda mabao 6-1, dhidi ya Majimaji, kasi tuliyokuwa nayo kipindi kile ndiyo imerudi upya na tunaweza kuwashangaza wengi Jumamosi,” alisema.
Hata hivyo kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Azam FC, Stewart Hall amesema wapo tayari kwa mapambano na hakuna timu itakayowatisha mbele yao. “Tumejipanga vyema na tuna uhakika kila atakayejitokeza mbele yetu tutamfunga,” alisema kocha huyo.
Mabingwa watetezi, Yanga SC wao leo watakuwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kumenyana na timu ngumu, MGambo JKT ya Kabuku, Tanga.
Naye Kocha Mkuu wa Yanga, Hans Pluijm amesema wanaenda Tanga kwa ajili ya kuivaa Mgambo Shooting wakiwa na matumaini makubwa ya kuibuka na ushindi. Pluijm amesema Yanga ina kila sababu ya kuibuka na ushindi kwani imeiva ikiwa na uhakika wa kuendelea kuwa mbele katika mbio za ubingwa.
Kocha Mkuu wa Mgambo, Bakari Shime amesema atawashangaza wadau wa soka kwa kuiadhiri Yanga kesho na kwamba hawatakuwa na utani. “Vijana wangu wapo tayari na wana kila sababu ya kufanya vizuri,” alisema kocha huyo.