UNAKUMBUKA wakati fulani yule kocha Mholanzi wa Yanga, Hans Pluijm, alishauri kinunuliwe kifaa fulani hivi cha mfumo wa elektroniki kwa ajili ya kupima ufanisi wa wachezaji wake uwanjani?
Ishu hiyo ikayeyuka Yanga baada ya jamaa kutemwa.
Sasa matajiri wa Azam FC wamekishusha kifaa hicho nchini na kimeanza
kufanya kazi.
Klabu hiyo pekee Afrika Mashariki ambayo uwanja
wake binafsi unakubalika kwa mechi za kimataifa, sasa inasubiri programu
maalumu ya Kijerumani ambayo itaunganishwa na kifaa hicho cha
‘Vis.Track Gps’ ambacho itakitumia kujua ufanisi wa kila mchezaji wake
uwanjani.
Vis.Track Gps kazi yake kubwa ni kupima takwimu za ufanisi wa mchezaji kuanzia mazoezini mpaka kwenye mechi.
Kwa mujibu wa Meneja wa Azam, Jemedari Said,
programu hiyo imeletwa na kocha wa vijana aliyekuwa anafanya mazoezi ya
vitendo katika klabu hiyo aitwaye Soren Lurz, raia wa Ujerumani.
“Soren ametupatia programu ambayo itatuwezesha
kufahamu ufanisi wa kila mchezaji uwanjani, hii tutaitumia haraka
iwezekanavyo pengine hata kabla ya ligi kuanza,” alisema Jemedari.
“Kila baada ya mechi tutakuwa tunafanya tathmini
kwa kutumia taarifa kutoka kwenye kompyuta hapo tutajua kila kitu na
kukifanyia kazi kiufundi.”
Alisema kifaa hicho kitatoa taarifa ya umbali
aliokimbia mchezaji uwanjani, muda aliokaa na mpira na idadi ya mashuti
aliyopiga hivyo kila mchezaji atajua utendaji wake.
Kifaa cha Vis.Track Gps kinaweza kupachikwa katika
jezi ya mchezaji au taarifa kuingizwa katika kompyuta na kumfuatilia
kila mchezaji uwanjani. Klabu nyingi za Ulaya hutumia teknolojia hii
kupima ufanisi wa mchezaji uwanjani.
Awali Yanga ilikuwa na mpango wa kutumia kifaa hicho chini ya Pluijm lakini mpango huo uliyeyuka baada ya kocha huyo kutemwa.
source.www.mwanaspoti.co.tz
source.www.mwanaspoti.co.tz
No comments:
Post a Comment