Rais wa Simba, Evans Aveva amemaliza utata wa usajili wa wachezaji wa kigeni uliokuwa umeigubika klabu hiyo kwa kusema Mkenya Donald Mosoti ndiye anabaki na Mrundi Butoyi Hussein wamempiga chini huku Yanga nao wakimpiga chini Emmanuel Okwi raia wa Uganda.
Simba na Yanga zimelazimika kufanya uamuzi mgumu
wa kupunguza idadi ya wachezaji wa kigeni ambao wamezidi katika klabu
zao kwa sababu usajili wa wachezaji katika klabu za Ligi Kuu Bara
unamalizika leo saa 6 usiku.
Akizungumza na chanzo chetu, Aveva alisema kuwa
Butoyi alikuja kwa ajili ya majaribio na si kusajiliwa hivyo mchezaji
atakayebaki ni Mosoti ambaye bado ana mkataba na klabu hiyo.
“Mosoti ni mchezaji wetu na ndiye atakayebaki,
sioni kama kuna sababu ya kufanya mabadiliko kwa sasa kwani hata kama
kocha angekuwa anamhitaji Butoyi angekuwa ameshatuambia, huyo alikuja
kwa ajili ya majaribio,” alisema Aveva.
Siku nzima ya jana viongozi wa Kamati ya Usajili
ya Simba walikuwa na vikao visivyomalizika ili kuhakikisha wanakamilisha
suala hilo, ambapo jana hiyo hiyo jioni walitakiwa kupeleka taarifa yao
ya usajili katika kikao cha Kamati ya Utendaji.
Kikao hicho cha Kamati ya Utendaji kilitarajiwa
kuongozwa na Aveva ili kufunga mjadala wa usajili wa wachezaji wao
watakaoitumikia klabu hiyo msimu ujao.
Habari kutoka visiwani hapa, ambapo Simba imeweka
kambi zinaeleza kwamba juzi Jumatatu usiku kocha Patrick Phiri alifanya
kikao na benchi la ufundi na kuwashirikisha juu ya uamuzi wake na wote
waliridhia kubaki kwa Mosoti.
Hata hivyo Phiri hakuwa tayari kuweka wazi juu ya
suala hilo huku akisema, “Nimetuma taarifa kwa viongozi wangu juu ya
mchezaji ninayemtaka, hivyo nasubiri majibu kutoka kwao, lakini sipendi
kufanya mambo kwa kukurupuka, kila kitu kifanywe kwa utaratibu.
“Nina mapendekezo yangu, lakini kabla hayajatolewa
uamuzi ni lazima yajadiliwe na viongozi ila lazima jibu lipatikane,”
alisema Phiri.
Kwa kukatwa Butoyi, wachezaji watano wa kigeni
waliobaki Simba ni Joseph Owino, Donald Mosoti, Amissi Tambwe, Pierre
Kwizera na Raphael Kiongera.
Kwa upande wa Yanga ambayop nayo ilikuwa na wachezaji sita wa kigeni, jumba bovu limemwangukia, Emmanuel Okwi.
Kwa mujibu wa chanzo hicho cha habari ni kwamba, uwezo na nafasi
wanazocheza wachezaji hao ni tofauti hivyo waliangalia mahitaji ya timu
wapi kwenye upungufu ili mmoja wao abakie. Kiiza anajulikana ni mzuri
zaidi anaposimama kati kama mshambuliaji na Okwi ni mzuri kucheza nyuma
ya straika au pembeni.
Yanga hivi sasa ina wachezaji wengi wa viungo
wenye uwezo wa kucheza winga kama, Andrey Coutinho, Simon Msuva, Haruna
Niyonzima, Nizar Khalfan, Omega Seme, Hamis Thabit, Hassan Dilunga.
Tofauti na ilivyo kwa washambuliaji wa kati ambao
ni Geilson Santos Santana ‘Jaja’, Said Bahanuzi, Jerry Tegete, Hussein
Javu na Kiiza.
Awali Hamis Kiiza ambaye pia ni raia wa Uganda
ndiye aliyekuwa anadaiwa kuachwa, lakini habari za ndani kutoka katika
klabu ya Yanga zinasema jumba bovu limemwangukia Okwi ambaye hadi jana
asubuhi alikuwa hajajiunga na timu.
No comments:
Post a Comment