Sunday, June 1, 2014
TAIFA STARS YAITOA ZIMBABWE NYUMBANI KWAO,BAADA YA KUTOKA SARE YA 2-2
Goooo!. Hivyo ndivyo watangazaji walitangaza mara nne katika uwanja wa Taifa wa Harare nchini Zimbabwe.
Taifa stars ya Mart Nooij itakabiliana na Msumbiji katika mchezo wa mwisho wa mtoano kuwania kupangwa hatua ya makundi kusaka tiketi ya fainali za mataifa ya Afrika mwakani nchini Morroco.
Hii imetokana na sare ya 2-2 waliyopata jioni hii dhidi ya wenyeji wao, timu ya taifa ya Zimbabwe.
Zimbabwe walioripotiwa kuwafanyia hujuma vijana wa Tanzania wameambulia patupu leo hii baada ya kuoneshwa soka safi na vijana wa Tanzania.
Haikutegemewa kuwa mechi ya mabao mengi kiasi hiki, lakini Zimbabwe ndio walianza kuamsha `mizimu` ya vijana wa Taifa stars waliokuwa wanamtazama kiongozi wao wa msafara, Rais wa TFF, Jamal Malinzi akiwa jukwaani.
Bao la dakika ya 10 walilopata Zimbabwe kupitia kwa Phiri Danisa liliwashitua mashabiki wa Tanzania, lakini nahodha wa Taifa Stars, Nadir Haroub Canavaro katika dakika ya 21 aliwazisha bao hilo na kuufanyaubao wa matangazo kusomeka 1-1 mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika.
Wakati Zimbabwe wakiwa katika presha ya kusaka bao la pili, dakika ya 46 kipindi cha pili walifanya makosa na Thomas Emmanuel Ulimwengu hakufanya makosa na kuwaadhibu goli la pili.
Dakika ya 55 kipindi hicho cha pili, Katsande Willard aliifungia Zimbabwe bao la pili la kusawazisha.
Baada ya hapo mpira ulianza kuchezwa kwa timu zote kutafuta mabao zaidi, lakini wenyeji ndio walikuwa kwenye presha kubwa zaidi kwasababu tayari Stars walikuwa na mtaji wa mabao zaidi.
Taifa stars ya Mart Nooij ilionesha kiwango safi na upinzani mkubwa ugenini na kuwafurahisha watanzania wachache waliokuwa uwanjani na waliokuwa wanaangalia kupitia televisheni.
Haikuwa kazi nyepesi kwa vijana wa Tanzania kuwafunga Zimbabwe, lakini jitihada kubwa walizofanya na kutambua kuwa mamilioni ya watanzania wapo nyuma yao, ilitosha kuwapa morali kubwa.
Mechi ya kwanza ambayo Stars ilishindi bao 1-0 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, tatizo kubwa lilionekana katika safu ya kiungo, lakini leo vijana walijidhatiti na kuonesha kandanda zuri.
Canavaro amekuwa kiongozi wa kuigwa kwani alionesha ushupavu wa kuwaelekeza njia wenzake ikiwemo kufunga bao muhimu la kusawazisha.
Beki kazi yake ni kulinda, inapofika wakati anafunga, basi amejiongezea majukumu kwa lengo la kuisaidia timu yake ipate mafanikio.
Kuwa nahodha sio kuvaa kitambaa tu bali ni pamoja na kuisaidia timu kama wanavyofanya akina Sergio Ramos. Kazi nzuri Nadir Haroub `Canavaro`.
Ulimwengu ni mchezaji wa TP Mazembe. Kuna faida ya kuwa na wachezaji wa kimataifa kama yeye. Kudhihirisha umuhimu wake, alifunga bao safi na kuwavusha watanzania hatua inayofauta. Kazi nzuri kijana.
Kwa matokeo ya leo, Taifa stars imefuzu hatua ya mwisho ya mtoano kwa wastani wa mabao 3-2 kuwania kupangwa hatua ya makundi kusaka tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika.
Hii inatokana na ushindi wa bao 1-0 iliopata uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam katika mchezo wa kwanza na matokeo ya 2-2 mjini Harare jioni hii.
Kwa maana hiyo, Taifa Stars inajiandaa kuutafuna mfupa wa Msumbiji katika hatua ya mwisho ya mtoano.
Msumbiji walifuzu hatua hiyo kwa wastani wa mabao 5-0 baada ya juzi kutoka suluhu ya bila kufungana na Sudan Kusini Ugenini, wakati waliibuka na ushindi mnono wa mabao 5-0 mjini Maputo.
Msumbiji wana historia ya kuwaharibia Taifa stars katika michezo muhimu ya mashindano, hivyo ni jukumu la wachezaji na kocha Nooij kupanga mikakati kabambe ya kuwanyamazisha `Mamba hao weusi`.
Mechi nyingine iliyomalizika jioni hii ni baina ya Lesotho na Liberia na kushuhudia Lesotho wakiibuka na ushindi wa mabao 2-0.
Mechi nyingine zinaendelea na utapata matokeo yake baadaye.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment