tuwasiliane

Wednesday, June 18, 2014

Robo tatu ya waliofaulu wachaguliwa kidato cha V


Robo tatu ya wanafunzi waliofaulu kidato cha nne kwa kupata daraja la kwanza hadi la tatu (Division I – III), wamechaguliwa kujiunga na kidato cha tano.
Idadi hiyo ya wanafunzi watakaojiunga katika shule za Serikali mwaka huu, imeongezeka kutoka 33,683 mwaka jana hadi kufikia 54, 085 sawa na asilimia 75.6 ya wanafunzi 71,527 wenye sifa ya kujiunga na kidato cha tano Tanzania Bara.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Kassim Majaliwa alisema kati ya waliochaguliwa wavulana ni 31,352 na wasichana ni 22, 733.
“Wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha tano 2014 ni kutoka shule za Serikali na zisizo za Serikali. Kati yao wavulana 14, 826 sawa na asilimia 27.41 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi na wengine 16, 526 sawa na asilimia 30.5 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi ya jamii,” alisema.
Alisema wasichana 7,859 sawa na asilimia 14.5 wamechaguliwa kusoma masomo ya sayansi na wengine 14, 874 sawa na asilimia 27.5 watajiunga na masomo ya sayansi ya jamii.
“Wanafunzi hao wamechaguliwa kujiunga kidato cha tano katika shule 241 zikiwamo 33 zilizopangiwa wanafunzi kwa mara ya kwanza mwaka huu,” alisema.
Mbali ya wanafunzi hao wanaojiunga kidato cha tano, Majaliwa alisema wengine 472 watajiunga na vyuo mbalimbali vya ufundi.
Alisema waliochaguliwa wanatakiwa kuripoti katika shule husika kuanzia Julai 10 na kwamba watatakiwa kufanya hivyo ndani ya siku 20 vinginevyo nafasi zao zitachukuliwa.
Kuhusu robo ya wanafunzi ambao walifaulu lakini hawakuchaguliwa, Majaliwa alisema hiyo ilitokana na ufinyu wa nafasi za shule na kukosa tahasusi (combination).
“Wanafunzi 16,800 wakiwamo watahiniwa wa kujitegemea 10 waliokuwa na sifa za msingi hawakuchaguliwa. Waliokosa kuchaguliwa kwa sababu ya ufinyu wa nafasi ni wanafunzi 16, 400 na wale kutokana na combination ni 400,” alisema.
Kuhusu wanaojiunga na vyuo vya ufundi, Majaliwa alisema idadi yao imepungua kutoka 530 mwaka jana hadi 472 mwaka huu kutokana na vyuo hivyo kuanza kudahili wanafunzi wa shahada ya kwanza.
Alisema kati ya hao waliochaguliwa, wavulana ni 355 na wasichana ni 117 na kwamba idadi ya wasichana imeongezeka kwa wanafunzi watatu kutoka 114 mwaka jana sawa na asilimia 2.63.
 Serikali inatarajia kufanya uchaguzi wa awamu ya pili baada ya kubaini nafasi zitakazokuwa wazi zinazotokana na wanafunzi ambao hawakuripoti awamu ya kwanza na imeweka utaratibu wa kuwapatia nafasi ya kusoma kidato cha tano na cha sita pamoja na stashahada ya elimu wanafunzi wenye sifa,” alisema

chanzo.www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment