tuwasiliane

Thursday, June 5, 2014

Kamwaga akimbia ofisi za Simba

 
Fukuto la uchaguzi linaloendelea ndani ya klabu ya Simba limemfanya Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Ezekiel Kamwaga kuiona ofisi yake chungu kama shubiri.
Kamwaga hajaingia ofisini kwa muda wa wiki moja sasa.
Jumatano ya wiki iliyopita, Kamwaga alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuzuiwa na kundi la wanachama wa ‘Simba la Taliban’ kuingia ofisini kwa kile walichodai kuwa wakati wa kutangazwa jina la Michael Wambura kuwa limeenguliwa kwenye mchakato wa uchaguzi kuwania urais wa Simba, katibu huyo alicheka.
Ilikuwa kama sinema, wanachama walipomzuia kuingia kupitia getini, Kamwaga akazunguka kwa mlango wa nyuma ambako kuna mgahawa wa Wasomali, akataka kuruka ukuta ili aingie ofisini,
lakini alikwama baada ya wanachama hao kumtoa mbio na kwenda kujisalimisha kituo cha Polisi Msimbazi.
Kamwaga aliomba msaada wa polisi ambao walifika klabuni hapo, hata hivyo waligonga mwamba kufungua ofisi hizo ambazo wanachama hao walikesha wakiilinda hadi Jumapili ambayo Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage alipokwenda kuifungua
.
“Kimsingi hakuna kitu kibaya nilichokifanya nawashanga wanachama kunizuia kuingia ofisini, tukio lile limenidhalilisha sana, naapa sitakanyaga tena ofisini,” alisema Kamwaga.
Hata hivyo, hatima ya Wambura kuendelea kwenye mchakato huo itajulikana Jumatatu wakati Kamati ya Rufani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) chini ya wakili, Julius Rugazia itakapokaa na kuipitia.
Wambura alikata rufani mapema wiki iliyopita, akipinga kuenguliwa katika mchakato wa uchaguzi ndani ya klabu ya Simba uliopangwa kufanyika Juni 29.
Wambura alienguliwa kwenye mchakato wa uchaguzi na Kamati ya Uchaguzi chini ya Wakili Damas Ndumbaro kwa kile kilichoelezwa kuwa si mwanachama wa Simba kwa kuwa alishavuliwa uanachama.
Ndumbaro pia alisema kamati yake ilipokea barua tatu tofauti ambazo moja kati ya hizo ameghushi saini ya aliyekuwa Katibu wa Simba, Evodius Mtawala.
Hata hivyo, wakati Wambura akisubiri hukumu yake Jumatatu, TFF imerudisha barua ya malalamiko ya Wambura na Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ na kuwataka kujipanga vizuri ili kufaili upya kesi yao katika Kamati ya Maadili ya TFF.
source.www.mwananchi.co.tz

No comments:

Post a Comment