HATIMAYE safari ya Mbeya City fc kwenda kushiriki michuano mipya ya CECAFA Nile Basin Cup nchini Sudan imekamilika baada ya kutumiwa tiketi za ndege.
Kocha msaidizi wa klabu hiyo Maka Mwalyisyi amezungumza na mtandao huu dakika chache zilizopita na kueleza kuwa wamepokea tiketi na wanaanza safari alfajiri ya kuamkia kesho na wanatarajia kufika Sudan kesho ijumaa majira ya saa 11:00 asubuhi kwa saa za huko.
Mwalwisyi amesema kwa mujibu wa Ratiba wanatakiwa kushuka dimbani kesho dhidi ya El Mereikh ya Sudan, lakini wapo katika mazungumzo ya kuomba kubadilishiwa ratiba kwasababu watakuwa wamechoka na safari.
“Tulitakiwa kucheza kesho. Lakini kuna mazungumzo yanaendelea ili kubadilishia ratiba. Kila kitu kinakwenda sawa na muda si mrefu tutaeleza kitakachojiri”. Amesema Mwalwisyi.
Hata hivyo, Mwalwisyi amesema wachezaji wote wapo katika hali nzuri na wamefurahi kuona safari imekamilika.
Mwalwisyi amesema kwa muda wote waliokuwepo Dar es salaam walikuwa wakifanya mazoezi katika uwanja wa Karume.
Licha ya kuchelewa kuondoka nchini, kocha huyo amesema sio kigezo cha kushindwa kufanya vizuri.
No comments:
Post a Comment