Wachezaji
wa kimataifa wa Tanzania wanaochezea TP Mazembe ya Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo (DRC), Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu
wanatarajiwa kuwasili Jumamosi mchana (Mei 17 mwaka huu) kujiunga na
Taifa Stars kwa ajili ya mechi dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors).
Washambuliaji hao watatokea moja
kwa moja Sudan ambapo kesho (Mei 16 mwaka huu) TP Mazembe itacheza mechi
ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya timu ya huko.
Ujio wa washambuliaji hao
utafanya wachezaji wote kutoka nje walioitwa na Kocha Mart Nooij kuwa
wamepatikana kwa ajili ya mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Afrika ambalo
fainali zake zitachezwa mwakani nchini Morocco. Mchezaji mwingine wan
je ambaye tayari ameripoti Stars ni Mwinyi Kazimoto anayecheza nchini
Qatar.
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) linamshukuru Mmliki wa TP Mazembe ambaye pia ni Gavana wa
Jimbo la Katanga, Moise Katumbi kwa kuwaruhusu wachezaji hao kujiunga
na Taifa Stars kwa vile mechi dhidi ya Zimbabwe ipo nje ya kalenda ya
FIFA.
Naye Kocha Nooij atakuwa na
mkutano na waandishi wa habari kesho (Mei 16 mwaka huu). Mkutano huo
utafanyika saa 5 kamili asubuhi kwenye kambi ya Taifa Stars iliyopo
katika hoteli ya Accomondia.
Wakati huo huo, Zimbabwe
inawasili usiku wa kuamkia Jumamosi (Mei 17 mwaka huu) ikiwa na msafara
wa watu 27. Timu hiyo itatua saa 7.30 usiku kwa ndege ya Ethiopian
Airlines na itafikia hoteli ya Sapphire Court iliyopo Mtaa wa Lindi, Dar
es Salaam.
Zimbabwe itafanya mazoezi siku
hiyo jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam tayari kwa mechi hiyo
itakayochezwa Jumapili saa 10 kamili jioni kwenye uwanja huo huo.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment